Breaking News

ACT WAZALENDO YAFAFANUA MARIDHIANO YA ZANZIBAR, YASEMA HAYABADILISHI MSIMAMO WA CHAMA BARA

Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Tanzania Bara, Isihaka Mchinjita, amesema tamko la maridhiano ya kisiasa kati ya chama hicho na CCM kwa upande wa Zanzibar limefikiwa baada ya takribani miezi minane ya mazungumzo yaliyofanyika kufuatia mvutano wa kisiasa uliozuka baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025

Mchinjita amesema kabla ya kufikiwa kwa maridhiano hayo, ACT Wazalendo ilisimama imara kutoshiriki Serikali ya Umoja wa Kitaifa hadi pale mazingira yatakapowekwa kuhakikisha serikali hiyo inatimiza madhumuni yaliyokusudiwa na Katiba ya Zanzibar.

Amesema kutokana na maswali na tafsiri mbalimbali zilizojitokeza kuhusu tamko hilo, chama kimeona ni muhimu kutoa ufafanuzi kwa wananchi, wadau wa demokrasia na Watanzania kwa ujumla kuhusu maana ya hatua hiyo na msimamo wake.

"Tamko hili linahusu mahsusi mchakato wa maridhiano ya kisiasa Zanzibar. Ndiyo maana tunaona ni muhimu wananchi wapate uelewa sahihi kuhusu kilichofikiwa na msimamo wa ACT Wazalendo," amesema Mchinjita.

Ameeleza kuwa Tanzania ni Jamhuri ya Muungano inayoundwa na Zanzibar na Tanzania Bara, huku akisisitiza kuwa historia na mazingira ya kisiasa ya Zanzibar yanatofautiana kwa kiasi kikubwa na yale ya Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa Mchinjita, Zanzibar imepitia hatua mbalimbali za kisiasa tangu mwaka 1995, hivyo suluhisho la changamoto zake linapaswa kuzingatia historia hiyo ya muda mrefu.

Aidha, amesema mbali na CCM, ACT Wazalendo ndicho chama pekee chenye ushawishi mkubwa katika Zanzibar na Tanzania Bara, jambo linalokipa nafasi ya kuelewa kwa undani historia na mwelekeo wa siasa za Zanzibar.

Amedai kuwa katika mazingira ya uchaguzi huru na wa haki, ACT Wazalendo imekuwa ikifanya vizuri Zanzibar, ikiwemo kushinda viti vya udiwani na ubunge katika maeneo mbalimbali ya Pemba na Unguja.

Mchinjita pia amesema ACT Wazalendo kimerithi harakati za kisiasa zilizokuwa zikiongozwa na Chama cha Wananchi (CUF) chini ya hayati Maalim Seif Sharif Hamad, hali inayokifanya kuwa sehemu ya historia ya mapambano ya demokrasia Zanzibar tangu mwaka 1995.

Amesisitiza kuwa uzoefu huo unakiwezesha chama kutafsiri kwa usahihi hali ya kisiasa ya Zanzibar na kushiriki kutafuta suluhisho la kudumu kwa changamoto zinazoikabili visiwa hivyo.