BRELA YAELEKEZWA KUWASAIDIA WAFANYABIASHARA MAONESHO YA SABASABA.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga ameielekeza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kuhakikisha inawatembelea wafanyabiashara wanaoshiriki Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba na kutoa usaidizi wa huduma zinazotolewa na BRELA.
Waziri Kapinga ametoa maelekezo hayo leo tarehe 01 Julai 2026 wakati alipotembelea banda la BRELA lililopo ndani ya jengo la Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na lile liliopo karibu na jengo la Wizara ya fedha kwenye maonesho ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam, Sabasaba.
“Hakikisheni mnatembelea mabanda ya wafanyabiashara na muwasaidie kurasimisha biashara zao, mjipange vizuri ili kuwawezesha na kutatua changamoto zao kwa maana sisi ni wawezeshaji wa biashara, msiende kama migambo nendeni kama wawezeshaji mkawasaidie.” Alisisitiza Mhe. Kapinga.
Aidha, katika hatua nyingine Waziri Kapinga ameitaka BRELA kuendelea kuwahudumia vizuri wananchi, wafanyabiashara na wadau wote wanaotembelea banda kupata huduma zinazotolewa bandani hapo.
BRELA inaeendelea kutoa huduma za papo kwa papo katika maonesho ya 50 ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yaliyoanza tarehe 28 Juni, 2026 ambapo wadau mbalimbali wamejitokeza kwa wingi kupata huduma kwa haraka, urahisi na uhakika kupitia mfumo ulioboreshwa wa BRELA Online Services (BOS).
Huduma zinazopatika katika banda la BRELA ni Usajili wa Jina la Biashara, Usajili wa Kampuni, Usajili wa Alama ya Biashara na Huduma, Utoaji wa Hataza, Utoaji Leseni za Biashara kundi A, Utoaji wa Leseni za Viwanda pamoja na huduma baada ya usajili.





