Breaking News

MCHENGERWA: MAKUBALIANO YA TANZANIA NA MAREKANI NI ALAMA YA UHURU, USAWA NA KUJITEGEMEA

Clements Robert, Dar es Salaam - Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa (Mb.), amesema Hati ya Ushirikiano wa Afya kati ya Tanzania na Marekani ni ishara ya mabadiliko makubwa ya kihistoria yanayoonesha Tanzania ya sasa ni taifa lenye uwezo wa kupanga, kugharamia na kusimamia mustakabali wake.

Akihusisha tukio hilo na historia ya uhusiano kati ya Tanzania na Marekani tangu mwaka 1963, Waziri Mchengerwa amesema mbegu iliyopandwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na aliyekuwa Rais wa Marekani, John F. Kennedy, imeendelea kukua na kuzaa ushirikiano wa heshima na usawa.

“Mwaka 1963 taifa changa lilipokelewa Ikulu ya Marekani kama taifa jipya linalotafuta nafasi yake duniani. Mwaka 2026 taifa hilo hilo linasaini makubaliano kama mshirika anayejitambua, anayefadhili mustakabali wake na anayesimamia maslahi yake mwenyewe,” amesema.
Waziri Mchengerwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake ulioiwezesha Tanzania kufikia hatua ya kuwa taifa lenye dira ya kujitegemea, afya bora na uchumi wa viwanda.

Pia amepongeza timu ya wataalamu wa Serikali iliyoongozwa na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Dawa na Vifaa Tiba, Bw. Emmanuel Tayari, kwa kazi kubwa ya kuhakikisha kila kipengele cha makubaliano hayo kinailinda Tanzania, rasilimali zake, taarifa zake na maslahi yake ya muda mrefu.