FCC YAWAHAMIZA WANANCHI KUTEMBELEA BANDA LAKE SABASABA KUPATA ELIMU NA HUDUMA ZA PAPO KWA PAPO
Dar es Salaam – Wananchi wamehimizwa kutumia fursa ya Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) kutembelea banda la Tume ya Ushindani (FCC) ili kupata huduma mbalimbali za papo kwa papo pamoja na elimu kuhusu ulinzi wa mlaji, ushindani wa biashara na udhibiti wa bidhaa bandia.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano kwa Umma wa FCC, Roberta Feruzi, aliyesema maonesho hayo yameiwezesha tume hiyo kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwapa elimu kuhusu haki zao pamoja na huduma zinazotolewa na taasisi hiyo.
Amesema FCC inatoa huduma mbalimbali katika banda lake, ikiwemo kupokea na kushughulikia malalamiko, usajili wa mikataba na huduma nyingine zinazolenga kuimarisha ushindani wa haki na kulinda maslahi ya walaji.
"Tunawaalika wananchi wote kufika katika banda la Wizara ya Viwanda na Biashara, ambalo ni banda jumuishi lenye taasisi zote zilizo chini ya wizara hiyo, ikiwemo FCC, ili wapate huduma na elimu kuhusu masuala ya ushindani, ulinzi wa mlaji na udhibiti wa bidhaa bandia," amesema Feruzi.
Ameeleza kuwa FCC haijajikita kutoa huduma ndani ya banda pekee, bali pia imeandaa programu ya kuwafuata wafanyabiashara na wajasiriamali katika maeneo mbalimbali ndani ya viwanja vya Sabasaba ili kuhakikisha elimu inawafikia wadau wengi zaidi.
Kwa mujibu wa Feruzi, tume hiyo imekuwa ikiendesha semina kwa makundi mbalimbali ya wafanyabiashara kuhusu sheria za ushindani, misingi ya ushindani wa haki na wajibu wao katika kulinda maslahi ya walaji.
Amesema tangu kuanza kwa maonesho hayo, zaidi ya wajasiriamali 700, wakiwemo wazalishaji wadogo na wa kati, wamefikiwa na kupatiwa elimu kuhusu ulinzi wa alama na nembo za biashara, kukuza ubunifu na kuongeza ushindani katika soko.
Aidha, amesema FCC inaendelea kuwalea vijana wabunifu wanaoshiriki maoneshoni kwa kuwapatia mwongozo wa namna ya kukuza biashara zao katika mazingira ya ushindani wa haki.
Feruzi amesisitiza kuwa kampeni ya utoaji elimu itaendelea hata baada ya kumalizika kwa Maonesho ya Sabasaba kupitia ofisi za FCC zilizopo Dar es Salaam na ofisi za kanda za Mwanza, Arusha, Mbeya na Dodoma.
Ameongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi jumuishi kwa kuweka mazingira bora ya biashara, huku FCC ikiendelea kuwa mlezi, mwezeshaji na mdhibiti wa ushindani wa haki nchini.
Amewahimiza wafanyabiashara, wabunifu na wananchi ambao hawajapata nafasi ya kutembelea maonesho hayo kufika katika ofisi za FCC zilizo karibu nao ili kupata elimu, ushauri na huduma mbalimbali kwa maendeleo ya biashara zao.




