Breaking News

GAVANA TUTUBA: UCHUMI WA TANZANIA UPO KWENYE MWELEKEO SAHIHI

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kiwango cha riba ya Benki Kuu cha asilimia 6.25 kilichotangazwa kwa robo ya tatu ya mwaka kitaleta utulivu wa bei, kuongeza ukwasi katika mabenki, kuchochea ukuaji wa mikopo na kuhakikisha mfumuko wa bei unaendelea kubaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5.

Akizungumza wakati wa kutembelea maonyesho ya kimataifa yanayoshirikisha zaidi ya mataifa 25, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba alisema hatua hiyo ni sehemu ya sera za fedha zinazolenga kuhakikisha uchumi unaendelea kuwa imara na shughuli za kiuchumi zinafanyika katika mazingira yenye utulivu.

Alisema kiwango hicho cha riba kimefikiwa baada ya tathmini ya kina ya hali ya uchumi na matarajio ya robo ya tatu ya mwaka, akibainisha kuwa kitasaidia kuwepo kwa fedha za kutosha katika sekta ya benki ili kuendelea kutoa mikopo kwa wananchi na wafanyabiashara.

Aidha, Tutuba alisema kipindi cha mavuno kinachotarajiwa kitasaidia kuimarisha thamani ya shilingi ya Tanzania, kuwawezesha wakulima kupata bei stahiki za mazao yao na kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni kupitia mauzo ya bidhaa nje ya nchi.

Kuhusu usimamizi wa sekta ya fedha, Gavana alisema Benki Kuu inaendelea kusimamia mabenki yote kwa ufanisi na kwamba yana mitaji ya kutosha, yanapata faida na yana ukwasi wa kutosha kuendelea kukopesha wananchi.

Akizungumzia maonyesho hayo, alisema ni jukwaa muhimu kwa Watanzania kujifunza teknolojia na mbinu mpya za shughuli za kiuchumi pamoja na kupata huduma na bidhaa kutoka ndani na nje ya nchi.

Alisema Benki Kuu imekuwa ikishiriki maonyesho hayo kila mwaka kwa lengo la kutoa elimu kuhusu sera za fedha, usimamizi wa sekta ya benki na umuhimu wa maamuzi ya sera za fedha katika kudhibiti mfumuko wa bei.

Gavana Tutuba alisema wananchi wengi waliotembelea banda la Benki Kuu walionesha hamu kubwa ya kupata ufahamu kuhusu masuala ya uchumi, hususan namna kiwango cha riba ya Benki Kuu kinavyoathiri uchumi na maisha ya kila siku.

Pia alibainisha kuwa wananchi wengi walipata elimu ya fedha kupitia mabanda mbalimbali, yakiwemo ya Wizara ya Fedha, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kijiji cha Bima, mabenki ya biashara na kampuni za simu.

Aliongeza kuwa Chuo cha Benki Kuu kimevutia idadi kubwa ya wananchi wanaotaka kujiendeleza katika elimu ya fedha, huku zaidi ya watu 200 wakijiandikisha kushiriki programu ya elimu ya kifedha (Financial Literacy) itakayofanyika mwezi Novemba.

Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kutembelea mabanda mbalimbali ili kupata elimu na huduma zitakazowawezesha kufanya maamuzi sahihi ya kifedha na kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi.