Breaking News

MAMIA YA WANANCHI WAENDELEA KUVUTIWA NA VIVUTIO VYA URITHI KATIKA BANDA LA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII SABASABA

Dar es Salaam - Mamia ya wananchi leo wameendelea kumiminika katika Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), wakionesha hamasa kubwa ya kujifunza na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii, historia na urithi wa taifa vinavyowasilishwa na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo.

Katika Banda la Makumbusho ya Taifa la Tanzania, wageni wamepata fursa ya kujifunza historia ya masalia ya mfupa wa dinosauri, asili na maendeleo ya utamaduni wa Waswahili, pamoja na urithi mwingine wa kihistoria na kiutamaduni unaobeba utambulisho wa Tanzania na kuvutia watalii kutoka ndani na nje ya nchi.
Mbali na utoaji wa elimu kwa umma, banda hilo pia limeshuhudia tukio muhimu la kukabidhiwa Ubalozi wa Hiari wa Utalii wa Tanzania kwa mwanautalii na mtangazaji wa vivutio vya utalii kutoka Oman, Khalid Hamed Al Barwani, aliyepata kutangaza kimataifa Shamba la Miti la Sao Hill baada ya kulitembelea mwaka 2024.

Ubalozi huo umekabidhiwa rasmi na Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ephraim Mafuru, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, ikiwa ni kutambua mchango wake mkubwa katika kuitangaza Tanzania kupitia majukwaa mbalimbali ya kimataifa.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa hadhi hiyo, Al Barwani alieleza dhamira yake ya kuendelea kuitangaza Tanzania kama moja ya nchi zenye vivutio vya kipekee duniani, huku akiwahamasisha watalii wengi zaidi kutembelea hifadhi za wanyamapori, maeneo ya kihistoria, urithi wa utamaduni na vivutio vingine vilivyopo nchini.

Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kutumia Maonesho ya Sabasaba kama jukwaa muhimu la kutangaza vivutio vya utalii, kutoa elimu kuhusu uhifadhi wa maliasili na urithi wa taifa, pamoja na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika maendeleo ya sekta ya utalii, kuelekea lengo la kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa na maandalizi ya AFCON 2027.