Breaking News

MRADI WA NJIA YA KUSAFIRISHA UMEME WA MSONGO WA KILOVOLTI 400 CHALINZE–DODOMA MBIONI KUKAMILIKA

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme ya Msongo wa Kilovolti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma uko kwenye hatua za mwisho za utekelezaji wake, huku ujenzi ukiwa umekamilika kwa asilimia 94 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 21, 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 28, 2026, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Bi. Irene Gowelle, amesema ili kuwezesha ukamilishaji wa kazi za mradi huo kutakuwepo na katizo la muda la umeme katika baadhi ya maeneo nchini kwa ratiba maalumu kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza itakua Julai 30 hadi Agosti 4 na ya pili itaanza Agosti 11 hadi 17, 2026.

Gowelle amesema hatua hiyo ni sehemu ya maandalizi ya ombi la Mkandarasi anayetekeleza mradi huo kampuni ya TBEA ambayo inalenga kuhakikisha kazi zinafanyika kwa hali ya usalama .
“Mradi huu umefikia hatua muhimu sana ya utekelezaji ambapo kipindi hiki, baadhi ya njia za kusafirisha umeme za kilovolti 220 na 132 zitalazimika kuzimwa kwa muda ili kuruhusu kazi za kuvuta na kuunganisha nyaya mpya kufanyika kwa usalama. Hii ni hatua ya kawaida katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu ya kusafirisha umeme na inalenga kukamilisha mradi huu wenye manufaa makubwa kwa Taifa,” amesema Bi. Gowelle.

Amefafanua kuwa baadhi ya maeneo katika mikoa iliyoko Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Magharibi na Kanda ya Kusini Magharibi inaweza kuathiriwa kwa nyakati tofauti kulingana na ratiba za utekelezaji wa kazi hizo.

Bi. Gowelle amesema TANESCO itaendelea kutoa taarifa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na majukwaa mbalimbali ya mawasiliano ili kuwawezesha wateja kupanga matumizi yao ya umeme kwa kuzingatia ratiba zitakazotolewa.

Aidha, amesisitiza kuwa Tanzania ina umeme wa kutosha na kwamba katizo hilo ni la muda, likiwa ni sehemu ya kukamilisha mradi huo wa kimkakati unaolenga kuimarisha uwezo wa usafirishaji wa umeme nchini. Ameongeza kuwa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara haitahusika katika ratiba hiyo ya katizo.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme ya Kilovolti 400 Chalinze–Dodoma, Mhandisi Newton Mwakifwamba, amesema mradi huo wenye urefu wa kilomita 345 na thamani ya takribani shilingi bilioni 514 umefadhiliwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema mradi unahusisha ujenzi wa njia mpya ya kusafirisha umeme pamoja na upanuzi wa vituo vya kupokea na kusambaza umeme vya Chalinze na Dodoma.
“Katika hatua hizi za mwisho, tutafanya kazi za kuvusha na kuunganisha njia mpya ya umeme katika maeneo ya Mkambarani, Kikombo na Mkonze. Hatua hizi ni muhimu ili kuhakikisha mradi unaanza kufanya kazi kwa ufanisi na usalama,” amesema Mhandisi Mwakifwamba.

Ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha uwezo wa mfumo wa taifa wa usafirishaji umeme na kuwezesha usafirishaji wa umeme unaozalishwa katika Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere kwenda maeneo mbalimbali ya nchi, hatua itakayoimarisha uhakika wa upatikanaji wa umeme na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.