Breaking News

RAIS SAMIA: MAWASILIANO YA SERIKALI NI NGUZO YA MAENDELEO NA ULINZI WA TAIFA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa mawasiliano ya Serikali yanahitaji uratibu, weledi na mwelekeo wa kimkakati ili kujenga imani ya wananchi kwa Serikali na kulinda maslahi ya Taifa.
 
Aidha alisema kuwa mawasiliano ni sehemu ya uongozi na nyenzo ya kimkakati ambayo ikitumika vizuri hujenga ushirikishwaji na kuwezesha taarifa za Serikali kutolewa kwa wakati, kwa lugha inayoeleweka na kwa takwimu zilizothibitishwa ili wananchi waweze kuelewa na kushiriki katika mipango ya maendeleo.

Rais Samia amesema hayo wakati akifungua Semina Elekezi ya Mawaziri, Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu Umuhimu wa Mawasiliano Serikalini, katika Ikulu ya Tunguu, Zanzibar. 

Semina hiyo ya siku mbili inawakutanisha kwa mara ya kwanza viongozi waandamizi wa Serikali kutoka pande zote mbili za Muungano kwa lengo la kujenga uelewa na msimamo wa pamoja kuhusu mawasiliano ya Serikali na umma.

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Rais Dkt. Samia alibainisha kuwa Serikali zote mbili zimepata mafanikio makubwa katika sekta za elimu, afya, miundombinu na nishati, mafanikio ambayo yanapaswa kuelezwa kwa wananchi kwa ufasaha mkubwa. 

Aligusia pia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 akieleza kuwa Serikali zimeanza kutekeleza mageuzi makubwa ya kiuchumi na huduma zinazowagusa wananchi moja kwa moja, ambapo takribani asilimia 70 ya utekelezaji wa Dira hiyo inategemea ushiriki wa sekta binafsi, hali inayohitaji mawasiliano na ushirikiano wa karibu sana kati ya Serikali na sekta hiyo.

Awali, akitoa utangulizi katika semina hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Mpogole Kusiluka, amesema kuwa mafunzo hayo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia ya kuwajengea viongozi uwezo katika mawasiliano ya Serikali na umma, yatakayojikita katika utoaji wa taarifa kwa ufasaha na kwa wakati pamoja na matumizi sahihi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii