Breaking News

PWANI KUANDAA MAONYESHO YA TANO YA UWEKEZAJI

DAR ES SALAAM – Mkoa wa Pwani unatarajia kuandaa Maonyesho ya Tano ya Uwekezaji yatakayofanyika Oktoba 5, 2026, yakilenga kutangaza fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji zilizopo mkoani humo.

Afisa Uwekezaji, Biashara na Viwanda wa Mkoa wa Pwani, Rehema Akida Mchumi, alisema hayo Julai 6, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Banda la Mkoa wa Pwani kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Aliwataka wawekezaji wa ndani na nje ya nchi pamoja na wafanyabiashara wadogo na wakubwa kutumia maonyesho hayo kufahamu na kuwekeza katika sekta mbalimbali zenye fursa kubwa za maendeleo.

Rehema alisema Mkoa wa Pwani umeendelea kuvutia uwekezaji katika sekta ya viwanda, hali iliyoongeza thamani ya mazao ya kilimo ikiwemo korosho, nazi, ufuta, mihogo, matikiti, mananasi, ndizi na machungwa kupitia shughuli za usindikaji.

Aliongeza kuwa uwekezaji katika usindikaji wa maziwa, utengenezaji wa saruji, bidhaa za chakula, vifungashio, ngozi, pamoja na uchakataji wa mazao ya misitu, magogo, samani na chumvi umechangia kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa mkoani humo.

Kwa mujibu wake, Mkoa wa Pwani pia umeendelea kuboresha miundombinu kwa kujenga nyumba za makazi, majengo ya ofisi, masoko ya kisasa, maduka makubwa, maghala, viwanja vya michezo, vituo vya mabasi, maegesho na dampo la kisasa.

Aidha, alisema kuna fursa nyingine za uwekezaji katika sekta ya madini kupitia uchimbaji na ujenzi wa mitambo ya kisasa ya kuchakata mawe, pamoja na sekta ya utalii ambapo hoteli, kumbi za mikutano, maeneo ya burudani na vivutio vingine vinaendelea kuimarishwa.

Rehema alisisitiza kuwa Mkoa wa Pwani una mazingira rafiki kwa uwekezaji na kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara kutumia fursa zilizopo kwa ajili ya kukuza biashara na uchumi.