Breaking News

TUZO YA SABASABA KUCHOCHEA HAMASA KWA WAWEKEZAJI KUSHIRIKIANA NA TBA

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umetumia mafanikio ya kupata tuzo ya mshindi wa pili wa Banda Bora katika sekta ya Miliki na Real Estate kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) kuwahamasisha wawekezaji kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP).

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud W. Kondoro, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa TBA, Bi. Amina Lumuli, alisema mafanikio hayo yanaonesha kuwa wananchi na wadau wameendelea kuvutiwa na fursa za uwekezaji pamoja na huduma zinazotolewa na wakala huo.

Alisema katika kipindi chote cha maonesho, TBA ilitoa elimu kuhusu miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa nchini na kuonesha namna sekta binafsi inavyoweza kushiriki katika utekelezaji wa miradi hiyo kupitia mfumo wa PPP.

Bi. Lumuli alisema wageni wengi waliotembelea banda la TBA walionesha kuvutiwa na miradi ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, majengo ya serikali pamoja na ukarabati na uboreshaji wa miundombinu ya michezo, ikiwemo Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Alieleza kuwa mwitikio huo unaipa TBA nguvu ya kuendelea kubuni miradi yenye tija inayochochea maendeleo ya sekta ya ujenzi na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Aidha, alisema tuzo hiyo ni uthibitisho wa kazi nzuri inayofanywa na watumishi wa TBA katika kuboresha huduma, kutumia ubunifu wa kihandisi na kusimamia miradi inayozingatia viwango vya ubora.

Bi. Lumuli aliwataka wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutumia fursa zilizopo kushirikiana na TBA katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa ushirikiano huo utachangia ukuaji wa uchumi na kuongeza huduma kwa wananchi.

TBA ilipokea tuzo hiyo katika sherehe za kufunga Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam zilizoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambapo taasisi hiyo ilishika nafasi ya pili katika kipengele cha Banda Bora upande wa Sekta ya Miliki na Real Estate.