BoT YAIKABIDHI HESLB URATIBU ZOEZI LA UPATIKANAJI WA WANUFAIKA WA MFUKO WA MWL. JULIUS NYERERE
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeikabidhi Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) jukumu la kusimamia mchakato wa maombi na uteuzi wa wanufaika wa Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Mwalimu Nyerere Memorial Scholarship Fund), hatua inayolenga kuongeza uwazi, usawa na ufanisi katika utoaji wa ufadhili kwa wanufaika wa elimu ya juu nchini.
Uamuzi huo umeanza kutumika katika udahili wa mwaka wa masomo 2026/27 baada ya Bodi ya Usimamizi wa Mfuko huo kuridhia kutumia mifumo ya HESLB katika mchakato wa kutangaza, kupokea na kuchakata maombi ya wanafunzi wanaostahili kupata ufadhili.
Hayo yamesemwa leo Agosti 28,2026 jijini Dar es Salaam na Gavana wa BoT, Bw. Emmanuel Tutuba wakati akizindua Mwongozo Mpya wa Utoaji Ufadhili kwa Wanafunzi wanaonufaika na Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Gavana Tutuba amesema, uamuzi huo ulifikiwa na Bodi ya Mfuko katika kikao chake kilichofanyika Mei,mwaka huu, baada ya kubaini umuhimu wa kutumia mifumo iliyopo serikalini ili kurahisisha mchakato wa kuwapata wanafunzi wenye sifa.
Amesema hapo awali, tangu mfuko huo ulipoanzishwa mwaka 2009, nafasi za ufadhili zilitangazwa kupitia vyombo vya habari, vikiwamo televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii, ambapo wanafunzi wenye sifa waliwasilisha maombi yao na kuchambuliwa na timu ya wataalamu wa BoT.
“Tumekubaliana sasa kutumia mifumo inayoratibiwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Mfumo huo una uwezo wa kutumia taarifa za ufaulu kutoka Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), hivyo kutuwezesha kupata wanafunzi wenye sifa kwa utaratibu wenye ufanisi zaidi,” amesema Gavana Tutuba.
Amesema,mabadiliko hayo yanaendana na msisitizo wa Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu umuhimu wa mifumo ya Serikali kusomana ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Gavana huyo, badala ya kuendelea na utaratibu wa kutangaza nafasi na kusubiri maombi, HESLB itaweza kutumia mifumo yake iliyopo kuchakata taarifa za wanafunzi na kubaini wanaokidhi vigezo vya ufadhili.
“Kwa kuwa mfumo wa Bodi ya Mikopo tayari unachakata taarifa za wanafunzi na kubaini wanaostahili kupata mikopo, tumeona ni jambo jema kutumia utaratibu huo huo katika kupata wanufaika wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere,” amesema
Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ulianzishwa Oktoba 12, 2009 ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuenzi mchango wa Baba wa Taifa katika kuendeleza elimu na rasilimali watu nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt.Bill Kiwia amesema, jukumu la kusimamia mchakato wa ufadhili huo ni heshima kubwa kwa taasisi hiyo na ni ishara ya imani iliyowekwa na BoT katika uwezo wa HESLB.
Dkt.Kiwia amesema, ushirikiano huo unaonesha namna taasisi za Serikali zinavyoweza kutumia mifumo na uwezo wao kwa pamoja ili kuboresha huduma kwa Watanzania.
“Leo historia inaandikwa. Bodi ya Mikopo imekabidhiwa jukumu la kutangaza na kupokea maombi ya ufadhili kwa ajili ya vijana wetu wa Kitanzania,”amesema.
Amesema,HESLB imewekeza zaidi ya dola milioni tano katika kujenga na kuimarisha mifumo yake ya kidijitali inayowezesha usimamizi wa mchakato mzima wa mikopo na ufadhili wa wanafunzi.
Miongoni mwa mifumo hiyo ni Mfumo wa Usimamizi wa Maombi Mtandaoni (OLAMS), unaotumika kupokea na kuchakata maombi ya wanafunzi.
Dkt.Kiwia amesema,mfumo mwingine ni Integrated Loan Management System (ILMS), unaowezesha kufuatilia mwanafunzi kuanzia anapoanza masomo, anapoendelea na masomo hadi anapohitimu na kuanza kurejesha mkopo
Amesema,HESLB pia imejenga mfumo wa kidijitali wa utoaji fedha kwa wanufaika pamoja na mfumo wa malipo ya marejesho unaounganishwa na Serikali e-Payment Gateway (GePG).
Pia,amesema taasisi hiyo imefikia kiwango cha takribani asilimia 98 cha matumizi ya mifumo isiyohitaji karatasi katika shughuli zake, jambo linalorahisisha utunzaji wa nyaraka na uchakataji wa taarifa.
Dkt.Kiwia amesema,HESLB imewezesha zaidi ya Watanzania milioni moja kupata elimu ya juu kupitia mikopo, huku zaidi ya Shilingi trilioni 9 zikitolewa kwa wanufaika.
Amesema,bodi hiyo pia imeendelea kusimamia programu nyingine za ufadhili, ikiwemo Samia Scholarship ambayo tangu ilipoanzishwa mwaka 2022 imewanufaisha zaidi ya wanafunzi 2,000 katika fani za Sayansi, Tiba, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati.










