MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI AMALIZA UTATA WA KISHERIA KUHUSU KITI CHA MAKAMU WA RAIS
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, amesema hakuna changamoto ya kikatiba kuhusu kujazwa kwa nafasi ya Makamu wa Rais, akieleza kuwa aliyekuwa Makamu wa Rais alipoteza sifa ya kushika nafasi hiyo baada ya kuvuliwa uanachama wa chama cha siasa.
Johari akizungumza leo Ijumaa Agosti 28, 2026 bungeni jijini Dodoma amesema anamfahamu Makamu wa Rais Mteule, Deogratius Ndejembi, kutokana na kufanya naye kazi, akimtaja kuwa ni mtu mwenye uwezo mkubwa, weledi, utiifu na nidhamu, pamoja na kuwa miongoni mwa watu wenye upendo na huruma.
Amesema kufuatia aliyekuwa Makamu wa Rais kuwasilisha taarifa ya kujiuzulu na baadaye kupoteza uanachama wa chama cha siasa, zimeibuka hoja za kikatiba kuhusu muda ambao kiti hicho kinakuwa wazi na utaratibu wa kujaza nafasi hiyo.
Johari amesema kwa mujibu wa Ibara ya 149(2) ya Katiba, taarifa ya kujiuzulu iliyotolewa na aliyekuwa Makamu wa Rais ingeifanya nafasi hiyo kuwa wazi tarehe 4 Septemba, kwa kuwa tarehe ya kujiuzulu ni siku taarifa inapokelewa au tarehe nyingine ya baadaye iliyotajwa katika taarifa hiyo.
Hata hivyo, amesema kabla ya tarehe hiyo kufika kulitokea jambo jingine la kikatiba, baada ya aliyekuwa Makamu wa Rais kuvuliwa uanachama wa chama cha siasa Agosti 26, 2026, hivyo kupoteza sifa mojawapo ya kushika nafasi hiyo.
Akifafanua hoja hiyo, Johari amesema tafsiri ya Katiba inapaswa kuzingatia misingi ya kisheria ya harmonious construction, ambayo inataka vifungu mbalimbali vitafsiriwe kwa kuzingatia uhusiano na maana ya Katiba kwa ujumla, badala ya kutazama kifungu kimoja pekee.
Amesema Ibara ya 47(4) inaweka sifa za mtu anayestahili kushika nafasi ya Makamu wa Rais, ikiwemo kuwa raia wa Tanzania, kutimiza umri wa miaka 40 au zaidi na kuwa mwanachama na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa.
Kwa msingi huo, amesema kupotea kwa sifa ya uanachama kabla ya tarehe ya kujiuzulu kuanza kutumika kulifanya suala la nafasi hiyo kuwa wazi na kutoa msingi wa kikatiba wa kuendelea na utaratibu wa kujaza nafasi hiyo kwa mujibu wa Katiba.
“Naliarifu Bunge lako Tukufu kuwa hakuna changamoto yoyote ya kikatiba,” amesema Johari.




