Breaking News

BRELA YATUMIA NANENANE KURAHISISHA USAJILI WA BIASHARA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma - Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umewataka wafanyabiashara, wakulima na wananchi kutumia Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Mzunguni, Dodoma, kupata huduma za urasimishaji wa biashara na kujifunza matumizi ya mfumo mpya ulioboreshwa wa usajili.

Akizungumza leo Agosti 1, 2026 katika banda la Wizara ya Viwanda na Biashara, Afisa usajili wa BRELA, Yusuph Mwasakafyuka Regio, alisema taasisi hiyo itatoa huduma mbalimbali katika maonesho hayo hadi Agosti 8, ikiwa ni sehemu ya kusogeza huduma karibu na wananchi.

Alisema huduma zinazotolewa ni pamoja na usajili wa majina ya biashara, usajili wa kampuni, utoaji wa leseni za biashara Kundi A, leseni za viwanda na usajili wa awali wa alama za biashara (trademark).

"Leo ukifika hapa unaweza kusajili jina la biashara, kampuni, kupata leseni ya biashara au kuanza mchakato wa usajili wa alama ya biashara bila kulazimika kufika ofisi za BRELA," alisema.

Regio alisema maonesho hayo pia yanatoa fursa kwa wafanyabiashara wanaokumbana na changamoto katika matumizi ya mfumo mpya wa usajili kupata msaada wa moja kwa moja kutoka kwa wataalamu wa BRELA.

Alisema mfumo huo umeboreshwa baada ya kubaini mapungufu yaliyokuwapo kwenye mfumo wa awali wa ORS, huku maboresho yakilenga kuongeza ufanisi, uwazi na usalama wa taarifa za kampuni.

Kwa mujibu wake, kupitia mfumo huo, huduma ambazo awali zilihitaji mteja kufika ofisini, kama uwasilishaji wa taarifa za dhamana (charges), sasa zinaweza kufanywa kwa njia ya mtandao kutoka mahali popote.

Aidha, alisema mfumo huo unamwezesha mteja kupata taarifa za kina kuhusu kampuni, ikiwemo hali ya uwasilishaji wa taarifa za mwaka (annual returns), pamoja na kuwapa wanahisa na wakurugenzi taarifa kila mabadiliko yanapofanyika ndani ya kampuni zao.

"Hii imeongeza usalama wa taarifa za kampuni kwa sababu wanahisa na wakurugenzi wote wanapata taarifa za mabadiliko yanayofanyika kwenye kampuni zao," alisema.

Alieleza kuwa ili kutumia mfumo huo mpya, mtumiaji anatakiwa kuwa na Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN), namba ya simu inayotumika na anuani sahihi ya barua pepe.

Regio aliwataka wafanyabiashara na wakulima wanaojihusisha na kilimo biashara kutumia fursa ya maonesho hayo kurasimisha shughuli zao ili kuongeza uaminifu katika masoko na kurahisisha upatikanaji wa fursa mbalimbali za biashara.