Breaking News

CHEN MINGJIAN: MASHINDANO YA 13 MPIRA WA KIKAPU DAR - BEIJING NI MFANO WA URAFIKI WA KWELI

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam – Jumamosi, 1 Agosti 2026: Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Mheshimiwa Chen Mingjian, amesema Mashindano ya 13 ya Mpira wa Kikapu ya Jamii ya Wachina ni mfano halisi wa urafiki wa kudumu uliopo kati ya Tanzania na China.

Kauli hiyo aliitoa wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo yaliyofanyika katika Viwanja vya Don Bosco, Namanga. Mashindano hayo yamedhaminiwa na Stanbic Bank Tanzania kwa Shilingi milioni 30 na kufunguliwa rasmi na Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Gerson Msigwa.

"Uhusiano kati ya China na Tanzania una historia ndefu na unaendelea kuimarika kupitia matukio kama haya ambapo michezo inatuunganisha katika roho ya urafiki na kuheshimiana. Mashindano haya ni ushuhuda kuwa ushirikiano wetu umefikia ngazi ya wananchi kwa wananchi," alisema Balozi Chen.
Katika hafla hiyo, Stanbic Bank ilikabidhi hundi ya udhamini wa Shilingi milioni 30. Mbali na udhamini, benki hiyo pia imetoa timu yake kushiriki mashindanoni, jambo lililoashiria dhamira ya kushirikiana kikamilifu na jamii ya Wachina.

Mkuu wa Kitengo cha Uwekezaji (Corporate and Investment Banking) wa Stanbic Bank Tanzania, Ester Manase, alisema benki imekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono mipango inayokuza mshikamano wa jamii.

"Kwa miaka mingi, mashindano haya yamekuwa moja ya majukwaa muhimu kwetu katika kuimarisha mahusiano na jamii ya Wachina nchini Tanzania kwa sababu tunaamini ushirikiano imara hujengwa kupitia uzoefu wa pamoja, si miamala ya kifedha pekee. Dhamira hiyo ndiyo msingi wa kazi yetu kupitia Standard Bank Group, ushirikiano wetu na ICBC pamoja na dawati letu maalum la huduma kwa wafanyabiashara wa Kichina," alisema Manase.
Manase aliongeza kuwa: "Udhamini wetu wa Shilingi milioni 30 una maana kubwa zaidi ya kugharamia mashindano. Kwa kushiriki kama mdhamini na pia mshindani, tunaonyesha kuwa ushirikiano wetu ni wa dhati na wa muda mrefu. Tunaendelea kuunga mkono mipango inayokuza mshikamano wa jamii, kubadilishana tamaduni na maendeleo ya pamoja."

Kwa upande wake, Bw. Gerson Msigwa alipongeza Stanbic Bank na jamii ya Wachina kwa kuendeleza utamaduni wa michezo unaoleta watu pamoja.

"Ushirikiano wa namna hii kati ya sekta binafsi na jamii unachangia kuimarisha mahusiano kati ya wananchi wa mataifa yetu mawili," alisema Msigwa.
Mashindano ya Mpira wa Kikapu ya Wachina yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kujenga mitandao ya biashara, kuimarisha mahusiano na kukuza kubadilishana uzoefu wa kitamaduni kati ya wadau kutoka Tanzania na China.

Kadri ushirikiano huo unavyoendelea kukua, Stanbic Bank itaendelea kuimarisha uhusiano wake na jamii ya Wachina nchini Tanzania pamoja na kuunga mkono majukwaa yanayochochea ushirikiano, maelewano na maendeleo ya pamoja.