CHONGOLO AHAMASISHA MATUMIZI YA TEKNOLOJI KUONGEZEKA TIJA KATIKA SEKTA YA KILIMO
Dodoma - Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amewataka wakulima na wadau wa sekta ya kilimo nchini kutumia kwa wingi teknolojia na matokeo ya tafiti zinazozalishwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) ili kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula na kukuza uchumi wa wananchi.
Waziri Chongolo alitoa wito huo Agosti 2, 2026, baada ya kuongoza mamia ya washiriki katika Marathon ya Maadhimisho ya Miaka 10 ya TARI iliyofanyika katika Viwanja vya Dkt. Samweli Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo.
Alisema katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, TARI imeendelea kutoa tafiti na ubunifu uliosaidia kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao, kuimarisha usalama wa chakula na kuwawezesha wakulima kutumia mbinu bora za kilimo.
Marathon hiyo iliwakutanisha viongozi wa serikali, watafiti, wadau wa sekta ya kilimo, wanamichezo na wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuhamasisha umuhimu wa utafiti katika kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na kuimarisha afya na mshikamano wa jamii.
Chongolo alisema mafanikio ya sekta ya kilimo yanategemea kwa kiasi kikubwa matumizi ya tafiti na teknolojia, hivyo akasisitiza wananchi kuendelea kushirikiana na TARI katika kuyafikisha matokeo ya tafiti kwa wakulima wengi zaidi.
Aliongeza kuwa maadhimisho ya miaka 10 ya TARI ni fursa ya kuonyesha mchango wa taasisi hiyo katika maendeleo ya sekta ya kilimo na kuhamasisha matumizi ya teknolojia zinazozalishwa na watafiti wa ndani.
Maadhimisho hayo yataendelea kwa shughuli mbalimbali zikiwemo maonesho ya teknolojia za kilimo, utoaji wa elimu kwa wananchi na huduma za ushauri wa kitaalamu kwa wakulima na wadau wa sekta ya kilimo.
TARI ilianzishwa kwa Sheria Na. 10 ya mwaka 2016 kwa lengo la kuratibu na kuendesha tafiti za kilimo zinazochochea maendeleo ya sekta hiyo na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.






