NIDC YAJIVUNIA DATA CENTER YA KISASA, YAHAMASISHA MATUMIZI YA CLOUD
DODOMA: Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data (NIDC) kimewahimiza Watanzania, wakiwemo taasisi, wafanyabiashara, wanafunzi na watafiti, kutumia huduma zake za Cloud Services zinazowezesha kuhifadhi taarifa na mifumo ya kidijitali ndani ya Tanzania kwa gharama nafuu huku zikihakikisha usalama wa taarifa.
Akizungumza katika Maonesho ya Kitaifa ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Ofisa wa TEHAMA wa NIDC, Alfred Abrahams Thawe, alisema huduma hiyo imeanzishwa mahsusi kuwahudumia Watanzania na kutoa fursa ya kuhifadhi na kusimamia taarifa za kidijitali kupitia miundombinu ya kisasa iliyopo nchini.
Alisema huduma hiyo inajumuisha Infrastructure as a Service (IaaS) inayowaruhusu taasisi, wanafunzi, watafiti na wajasiriamali kuhifadhi na kuendesha mifumo yao kwenye miundombinu ya NIDC bila kulazimika kujenga vituo vyao vya data.
Thawe alisema huduma nyingine ni Storage as a Service, inayowawezesha watumiaji kuhifadhi nyaraka, tafiti na taarifa mbalimbali kwa usalama kupitia mfumo wa Cloud, pamoja na DNS as a Service, unaorahisisha usimamizi wa majina ya tovuti na huduma nyingine za kidijitali kwa gharama nafuu.
Alieleza kuwa NIDC imejipambanua kwa kuwa na cheti cha viwango vya kimataifa (ISO Certification), huku kituo chake cha kuhifadhi data kikiwa ndani ya Tanzania, hatua inayohakikisha taarifa za Watanzania zinabaki na kuhifadhiwa nchini.
Aidha, alisema kituo hicho ni Tier 3 Data Center, kiwango kinachoonyesha ubora wa miundombinu yake ya kuhifadhi data. Alifafanua kuwa sababu pekee inayokifanya kisifikie kiwango cha Tier 4 ni kutegemea chanzo kimoja cha umeme kutoka TANESCO, licha ya miundombinu mingine kukidhi viwango vya juu.
"Kama tungekuwa na chanzo kingine cha umeme mbali na TANESCO, kituo chetu kingefikia kiwango cha Tier 4," alisema.
Thawe alisema huduma za NIDC zinapatikana kupitia tovuti ya taasisi, ambapo wananchi wanaweza kujisajili kwa kutumia majina na anuani ya barua pepe kwa huduma za Cloud, huku baadhi ya huduma za biashara zikihitaji taarifa kama namba ya TIN.
Aliongeza kuwa ada ya kuanza kutumia huduma za Cloud ni Sh49,999, akisema kiwango hicho ni rafiki na kinakusudia kuwapa Watanzania wengi zaidi fursa ya kutumia huduma za kisasa za kuhifadhi taarifa na mifumo ya kidijitali.





