CHUO CHA USTAWI WA JAMII CHATANGAZA KOZI MPYA, UDAHILI NA USHAURI NASAHA NANENANE
DODOMA: Chuo cha Ustawi wa Jamii kimesema kimejipanga kuandaa wataalamu watakaochangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuanzisha na kuimarisha kozi zinazolenga afya ya akili, utatuzi wa migogoro, maendeleo ya watoto na uongozi wa rasilimali watu.
Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa yanayoendelea mkoani Dodoma, Mhadhiri wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Debora Alexander Bwana, alisema chuo hicho kinatoa huduma tatu muhimu katika banda lake ambazo ni kutangaza kozi zinazotolewa chuoni, kutoa huduma za ushauri na unasihi, pamoja na kufanya udahili wa wanafunzi wenye sifa za kujiunga na masomo.
Alisema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kujenga taifa lenye ustawi, haki na kujitegemea, hivyo chuo kimeboresha programu zake ili kuwapa wanafunzi maarifa na ujuzi wa kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.
Bwana alisema miongoni mwa kozi mpya ni Saikolojia, ambayo inalenga kuzalisha wataalamu wa afya ya akili watakaosaidia kutatua changamoto za kisaikolojia katika jamii, pamoja na kozi ya Conflict Management and Alternative Dispute Resolution inayowajengea wanafunzi uwezo wa kusuluhisha migogoro kabla haijafikishwa mahakamani.
Aidha, alisema chuo kinatoa kozi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto inayowawezesha wahitimu kujiajiri kwa kuanzisha vituo vya kulelea watoto (daycare) au kuajiriwa katika taasisi zinazohudumia watoto.
Alitaja kozi nyingine zinazotolewa kuwa ni Human Resources Management, Community Work with Children and Youth, Business Administration, Entrepreneurship and Marketing, Labor Laws pamoja na Labor Relations and Public Management.
Kwa mujibu wake, kozi hizo zinapatikana kuanzia ngazi ya Cheti (Certificate), huku baadhi zikitolewa hadi ngazi ya Shahada ya Uzamili (Master's), ikiwemo Human Resources Management, Social Work na Labor Relations.
Bwana alisema kuanzia mwaka huu chuo kitaanza kutoa masomo ya Shahada ya Uzamili kwa njia ya mtandao (online), hatua itakayowawezesha wanafunzi kusoma wakiwa mahali popote walipo.
Aliwataka wananchi na wahitimu wanaotafuta fursa za masomo kutembelea banda la Chuo cha Ustawi wa Jamii katika Maonesho ya Nanenane ili kupata elimu zaidi kuhusu kozi, huduma za ushauri na kufanya udahili.




