Breaking News

ASILIMIA 90 YA CHAI YA TANZANIA INAUZWA NJE, BODI YAHAMASISHA WATANZANIA KUWEKEZA KWENYE SEKTA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma - Bodi ya Chai Tanzania imewahamasisha Watanzania kuongeza matumizi ya chai pamoja na kuwekeza katika sekta hiyo, ikisema unywaji wa chai nchini bado ni mdogo licha ya faida zake kiafya na fursa zilizopo katika biashara ya zao hilo.

Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa yanayoendelea jijini Dodoma, Afisa Mkuu wa Mipango na Uhamasishaji wa Bodi ya Chai, Godlove Mwinga, alisema taasisi hiyo inayosimamiwa na Wizara ya Kilimo imetumia maonesho hayo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa chai na fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta hiyo.

Alisema tafiti zinaonesha kuwa asilimia 10 pekee ya chai inayozalishwa nchini ndiyo inayotumika ndani ya Tanzania, huku asilimia 90 ikiuzwa katika masoko ya nje, ikiwemo Ulaya, Marekani na Asia.

“Watanzania wengi bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu faida za chai. Nje ya nchi chai yetu inahitajika sana kwa sababu ni chai ya asili (organic) na haina mabaki makubwa ya kemikali,” alisema Mwinga.

Kwa mujibu wa Mwinga, chai ina kemikali ya asili inayojulikana kama polyphenol, ambayo husaidia mwili kupambana na magonjwa mbalimbali. Alieleza kuwa matumizi ya chai yanaweza kusaidia kuimarisha afya ya figo, kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo, kusaidia afya ya kinywa na meno, pamoja na kusaidia mwili kuondoa uchovu.

Aliongeza kuwa chai pia ina mchango katika ustawi wa akili kwa kusaidia kupunguza msongo wa mawazo na kuongeza utulivu wa kiakili.

Mbali na matumizi ya chai, Mwinga aliwataka Watanzania kutumia fursa zilizopo katika uwekezaji wa sekta hiyo kupitia kilimo cha chai, uanzishaji wa viwanda vya kuchakata chai, biashara ya kuchanganya chai (blending), pamoja na biashara ya ndani na usafirishaji wa chai nje ya nchi.
Alisema sekta ya chai ina nafasi kubwa ya kuongeza ajira, mapato na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa ikiwa wananchi wengi zaidi watawekeza katika shughuli za uzalishaji na biashara ya zao hilo.

Kuhusu mikakati ya kuongeza matumizi ya chai nchini, Mwinga alisema Bodi ya Chai inaendelea kutoa elimu kupitia vyombo vya habari na kushiriki maonesho mbalimbali yakiwemo Nanenane, Sabasaba na matukio mengine ya kitaifa.

Akizungumzia historia ya zao la chai nchini, alisema chai ililetwa Tanzania na Wajerumani mwaka 1902 na Tanzania kuwa nchi ya kwanza Afrika Mashariki kulima zao hilo, kabla ya Kenya mwaka 1903 na Uganda mwaka 1905. Uzalishaji wa kibiashara ulianza mwaka 1926 katika maeneo ya Rungwe na Njombe.

Kwa mujibu wa Bodi ya Chai, kuongeza matumizi ya chai ndani ya nchi kutasaidia kuboresha afya za wananchi, kuongeza nguvu kazi na kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa.