DIB: AMANA ZA HADI MILIONI 7.5 ZINALINDWA, WATEJA WA FBME BANK WAHIMIZWA KUFUATILIA SALIO LA FEDHA
DODOMA: Bodi ya Bima ya Amana (DIB) imesema amana za wateja katika benki na taasisi za fedha zilizopewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinalindwa kwa kiwango cha hadi shilingi milioni 7.5 endapo benki itafilisika au kufutiwa leseni.
Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa DIB, Lwaga Mwambande, alisema kiwango hicho kinahakikisha mteja mwenye amana zisizozidi shilingi milioni 7.5 analipwa fedha zake zote ikiwa benki yake itafungwa.
Alisema mfuko wa bima ya amana huchangiwa na benki na taasisi za fedha zinazopokea amana kutoka kwa wananchi, ambapo kila benki huchangia asilimia 0.15 ya jumla ya amana zake mara moja kwa mwaka.
Mwambande alisema fedha zinazokusanywa huwekezwa katika dhamana za Serikali na maeneo mengine ya uwekezaji ili kuhakikisha mfuko unakuwa na uwezo wa kulipa fidia kwa wateja pale benki inaposhindwa kuendelea na shughuli zake.
Alifafanua kuwa wateja wenye fedha zinazozidi kiwango cha kinga hawapotezi haki zao, kwani baada ya kulipwa fidia huendelea kudai salio lao kupitia mchakato wa ufilisi unaosimamiwa na Bodi ya Bima ya Amana kwa niaba ya Benki Kuu ya Tanzania.
Alisema kwa sasa Bodi inaendesha ufilisi wa benki tisa zilizofungwa kati ya mwaka 2000 na 2018 ambazo ni Greenland Bank, Delphis Bank, FBME Bank, Efatha Bank, Covenant Bank for Women, Mbinga Community Bank, Njombe Community Bank, Meru Community Bank na Kagera Farmers Cooperative Bank.
Kwa mujibu wa Mwambande, pamoja na kulipa fidia na kusimamia ufilisi, DIB pia imeanza kutekeleza jukumu la kusaidia benki zinazokabiliwa na changamoto za kifedha ili kupunguza hasara na kuzuia kufungwa kwa taasisi hizo. Alisema hatua hiyo inaweza kujumuisha kutoa dhamana au mikopo kwa benki husika kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania.
Alibainisha kuwa majukumu makuu ya DIB ni kukusanya michango ya wanachama wake, kuwekeza fedha za mfuko wa bima ya amana, kulipa fidia kwa wenye amana, kusimamia ufilisi wa benki zilizofungwa na kupunguza hasara kwa benki zinazokumbwa na changamoto za kifedha.
Kwa upande wake, Meneja wa Fedha na Uhasibu wa DIB, Romuli Mtui, alisema ufilisi wa benki saba zilizofungwa mwaka 2017 na 2018 bado unaendelea katika hatua mbalimbali.
Mtui alisema DIB hivi karibuni ilitangaza malipo ya mwisho kwa baadhi ya waliokuwa wateja wa FBME Bank Tanzania na kuwataka waliohusika kufuatilia salio la fedha zao katika ofisi za Bodi zilizopo ndani ya majengo ya Benki Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam na Dodoma, au kupitia namba za mawasiliano zilizopo kwenye tovuti ya taasisi hiyo.
Aliwataka pia wateja ambao bado hawajachukua fidia ya amana zao kufika katika matawi ya Benki ya Biashara au Tanzania Commercial Bank (TCB) ili kupokea malipo yao.
Aidha, alisema wateja waliokuwa na amana zilizozidi kiwango cha fidia kilichokuwa kinatumika wakati benki hizo zilipofungwa wanapaswa kuendelea kufuatilia malipo ya salio lao kupitia Bodi ya Bima ya Amana wakati mchakato wa ufilisi ukiendelea.
Mtui alisema hadi sasa zaidi ya shilingi bilioni 2.9 za fidia ya amana bado hazijachukuliwa na wateja, hivyo akawahimiza wahusika kujitokeza ili kukamilisha taratibu za malipo





