WAANDISHI WA HABARI WAPONGEZWA KWA KUONGOZA MAPINDUZI YA MATUMIZI YA BIMA
Dodoma - Waandishi wa habari nchini wamepongezwa kwa kujitokeza kwa wingi kukata bima za maisha na mali katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, hatua iliyoelezwa kuwa ni mfano bora kwa wananchi katika kujenga utamaduni wa kujilinda dhidi ya majanga mbalimbali.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa Shirika la Bima la Taifa (NIC Insurance), Karimu Meshack, amesema waandishi wa habari wameonyesha uelewa mkubwa kwa kuamua kutekeleza kile ambacho kwa muda mrefu wamekuwa wakikihamasisha kwa jamii kupitia kazi zao.
Meshack alisema ndani ya siku moja pekee waandishi wa habari 11 walikata bima za maisha na mali, jambo alilosema linaonyesha mabadiliko makubwa ya mtazamo kuhusu umuhimu wa bima kwa watu wanaofanya kazi zenye mazingira yenye hatari na changamoto mbalimbali.
Alisema waandishi wa habari ni daraja muhimu la kuwafikishia wananchi elimu ya bima, hivyo uamuzi wao wa kujiwekea kinga ya kifedha unawapa nguvu ya kuzungumza kwa uzoefu na kuwa mfano wa kuigwa na makundi mengine ya jamii.
Aidha amewahimiza waandishi wengine kote nchini kuufuata mfano huo kwa kutambua kuwa, pamoja na taaluma yao ya kuhabarisha umma, wao pia ni wazazi, walezi na wategemezi wa familia wanaohitaji ulinzi wa maisha na mali zao.
Nao baadhi ya waandishi waliokata bima walisema wameamua kufanya hivyo ili kuhakikisha familia zao zinakuwa salama endapo yatatokea majanga yasiyotarajiwa, huku wengine wakichagua bima za nyumba na mali kwa lengo la kulinda vitega uchumi walivyovijenga.
Meshack amesema ongezeko la waandishi wanaokata bima linaunga mkono jitihada za Serikali za kuongeza ushiriki wa wananchi katika huduma za bima, akisisitiza kuwa kulinda maisha na mali ni msingi wa kulinda uchumi wa familia na taifa kwa ujumla.
Aidha ametoa wito kwa wananchi wote kuiga mfano wa waandishi wa habari kwa kujitokeza kukata bima mbalimbali kulingana na mahitaji yao, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kujenga jamii yenye usalama wa kifedha na kuongeza ustahimilivu dhidi ya majanga yasiyotarajiwa.




