DIB: BILIONI 4 ZA WATEJA WA FBME BADO HAZIJACHUKULIWA, WADAI WENGINE WATAKIWA KUSUBIRI KUKAMILIKA KWA UFUATILIAJI WA MALI
Dodoma - Bodi ya Bima ya Amana (DIB) imewataka wateja wa Benki ya FBME wenye amana ambao bado hawajajitokeza kudai fedha zao kufanya hivyo haraka, ikieleza kuwa takribani Sh bilioni 4 bado zinasubiri kulipwa kwa wateja 428.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Bima ya Amana, Isack Kiwili, wakati akizungumza na wananchi waliotembelea banda la taasisi hiyo katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma.
Kiwili alisema madai yote ya wenye amana wa FBME kwa upande wa Tanzania yalikuwa zaidi ya Sh bilioni 35, yakihusisha wateja kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Alisema hadi sasa DIB imelipa asilimia 85 ya madai hayo, huku kiasi kilichosalia cha takribani Sh bilioni 4 kikiwa hakijachukuliwa kutokana na baadhi ya wanufaika kutokujitokeza.
"Kwa sasa wateja 428 bado hawajajitokeza kudai fedha zao. Tunawahimiza wafike kujaza fomu na kukamilisha taratibu ili walipwe, kwa sababu fedha hizo zipo na ni haki yao," alisema.
Alifafanua kuwa baada ya wateja wote wanaostahili kulipwa kukamilishiwa malipo ya awamu zilizopita, DIB itaendelea na hatua ya kulipa asilimia 15 iliyobaki ili kukamilisha malipo yote ya madai ya wenye amana, ambayo kwa ujumla wake yanafikia zaidi ya Sh bilioni 35.
Kuhusu kundi la wadai wasiokuwa wenye amana, Kiwili alisema hawatalipwa katika awamu ya sasa kwa kuwa DIB inaendelea kufuatilia mali za benki hiyo ili kupata fedha za kutosha za kulipa madai yao.
Alieleza kuwa kundi hilo linajumuisha wadai mbalimbali, ikiwemo baadhi ya wafanyakazi waliowahi kufungua kesi mahakamani kuhusu madai yao ya kisheria.
"Hawa wadai wasubiri. DIB inaendelea kufuatilia mali za FBME na pindi fedha za kutosha zitakapopatikana tutatangaza rasmi utaratibu wa kuwalipa kulingana na kiwango kitakachopatikana," alisema.
Aidha, Kiwili alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuweka fedha zao katika benki na taasisi za fedha zenye leseni ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), akisema hatua hiyo ndiyo inayowapa kinga ya kufidiwa endapo taasisi husika itafilisika au kufungwa.
Alisema mfano wa FBME unaonesha umuhimu wa kuweka fedha katika taasisi zilizosajiliwa na zenye leseni, kwani kama fedha hizo zingewekwa katika taasisi zisizo rasmi, wateja wasingeweza kupata fidia inayotolewa na DIB.
Pia aliwaalika wananchi kutembelea banda la Bodi ya Bima ya Amana katika Maonesho ya Nanenane ili kupata elimu kuhusu majukumu ya taasisi hiyo na taratibu za ulinzi wa amana za wateja wa taasisi za fedha.




