TAMKU YATANUA HUDUMA KWA WAKULIMA, YAJIPANGA KUJENGA KIWANDA CHA KOROSHO,
Dodoma. Chama Kikuu cha Ushirika cha TAMKU kimesema kinaendelea kupanua huduma kwa wakulima kupitia uwekezaji katika usafirishaji wa mazao, mfumo wa stakabadhi ghalani na mpango wa kujenga kiwanda cha kuchakata korosho wilayani Tunduru, hatua inayolenga kuongeza thamani ya mazao na mapato ya wanachama.
Mjumbe wa Bodi ya TAMKU, Nurudini Rajabu Chikolo, alisema hayo katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane, akieleza kuwa chama hicho pia kinatarajia kujenga jengo la utawala la ghorofa tano litakalogharimu takribani Sh bilioni saba pamoja na ukumbi wa kisasa wenye uwezo wa kuhudumia zaidi ya watu 700.
Alisema maandalizi ya utekelezaji wa miradi hiyo yamefikia hatua nzuri baada ya kukamilika kwa taratibu za vibali na maandalizi ya ramani za uhandisi, huku ujenzi ukitarajiwa kuanza mara taratibu zilizosalia zitakapokamilika.
Kwa mujibu wa Chikolo, TAMKU imeendelea kuimarisha huduma kwa wakulima kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani unaohudumia mazao ya korosho, ufuta na mbaazi katika Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma pamoja na maeneo jirani, ikiwemo Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe.
Alisema chama hicho pia kinamiliki kampuni tanzu ya TAMKU Group of Companies Limited inayosimamia maghala ya kuhifadhi mazao, kupokea mazao ya wakulima na kusambaza pembejeo za ruzuku, hatua inayosaidia kuongeza uzalishaji na kipato cha wakulima.
Mbali na hilo, alisema TAMKU imewekeza katika sekta ya usafirishaji kwa kumiliki malori matano yanayotoa huduma za usafirishaji wa mizigo nchini kote, jambo linalorahisisha usafirishaji wa mazao na kupunguza gharama kwa wakulima.
Akizungumzia ushiriki wa vijana, Chikolo aliwataka kujiunga na vyama vya ushirika, akisema mfumo huo unatoa fursa za kujikwamua kiuchumi kupitia uzalishaji, masoko na uwekezaji wa pamoja.
Pia aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kutoa pembejeo za ruzuku kwa wakulima, akisema hatua hiyo imechangia ongezeko la uzalishaji wa korosho wa TAMKU kutoka tani 17 mwaka 2017 hadi tani 41,000 katika msimu uliopita.
Alisema chama hicho kinatarajia kuongeza zaidi uzalishaji katika msimu ujao kupitia uwekezaji unaoendelea na kuimarisha huduma kwa wakulima.




