DOROTHY SEMU: VIJANA WAPIGANIE KATIBA MPYA YA WANANCHI
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Dorothy Semu, amewataka vijana nchini kusimama imara katika kudai Katiba mpya ya wananchi, akisisitiza kuwa mchakato huo haupaswi kuwa wa viraka wala kuendeshwa kwa maslahi ya chama au kundi fulani.
Semu aliyasema hayo leo jijini Dar es Salaam katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yaliyoandaliwa na Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalendo, ambapo amesema vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kupigania mabadiliko ya kisiasa na kikatiba nchini.
Amesema ACT-Wazalendo inataka Katiba mpya itakayorejesha mamlaka ya maamuzi kwa wananchi, kulinda maslahi ya taifa na kuhakikisha vijana wanapata haki na fursa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo ajira, mtaji, elimu, haki ya kujieleza, haki za kisiasa na huduma bora za jamii.
“Tunataka Katiba ya wote kwa maslahi ya wote. Hatutaki Katiba itakayoweka viraka au kufanyiwa matengenezo kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi. Tunataka Katiba itakayowasilisha sauti za Watanzania wote,” amesema Semu.
Aidha, ameeleza kuwa chama hicho kinataka mchakato wa Katiba mpya uanze kwa kufanya marekebisho ya sheria zinazohusika na mchakato huo, kisha kuitishwa kwa mkutano wa kitaifa utakaowakutanisha wadau mbalimbali kujadili masuala muhimu na kuweka msingi wa makubaliano ya kitaifa.
Kwa mujibu wa Semu, baada ya hatua hiyo, kunapaswa kuundwa kamati ya wataalamu itakayokusanya maoni mbalimbali, yakiwemo yaliyowahi kutolewa na Tume ya Jaji Warioba pamoja na rasimu ya Katiba ya mwaka 2014, ili kuandaa rasimu ya Katiba mpya itakayopigiwa kura ya maoni.
Semu pia amewataka vijana kujielimisha kuhusu Katiba iliyopo, rasimu mbalimbali na masuala ya kitaifa ili wawe sehemu ya mjadala wa mchakato wa Katiba mpya badala ya kuwa watazamaji.
“Vijana msiogope wala msitishwe. Ninyi ndiyo tunawategemea kuleta mabadiliko katika taifa hili. Tunataka vijana muwe na ajenda yenu katika Katiba mpya na msinunuliwe wala kupelekwa na upepo wa kisiasa,” amesema.
Katika hatua nyingine, Semu amesisitiza msimamo wa ACT-Wazalendo kuhusu matukio ya baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, akisema chama hicho kinataka kuachiwa huru kwa wafungwa wote wa kisiasa na kufutwa kwa kesi zinazohusishwa na masuala ya uasi na uchaguzi mkuu.
Amesema pia chama hicho kinataka mchakato wa maridhiano ya kitaifa ujikite katika misingi ya ukweli, haki na uwajibikaji, pamoja na kuwepo kwa tume huru ya uchunguzi itakayochunguza matukio yaliyotokea Oktoba 29 na siku zilizofuata.
Semu amesisitiza kuwa kupata Katiba mpya si zawadi kutoka kwa watawala, bali ni jukumu la kizazi cha sasa kuipigania kwa njia za kikatiba na kuhakikisha inakuwa Katiba inayolinda haki na maslahi ya wananchi.
Amewataka vijana wa ACT-Wazalendo kuendeleza utamaduni wa kukutana, kusikilizana na kujadili changamoto zao katika ngazi zote kuanzia taifa, mikoa, majimbo, kata hadi matawi, ili maoni yao yawe sehemu ya maamuzi ya chama na taifa.




