Breaking News

e-GA YAWEKA BAYANA MCHANGO WAKE KATIKA MAPINDUZI YA KILIMO NCHINI

Na Mwandishi Wetu, Dodoma - MAMLAKA ya Serikali Mtandao (e-GA) imesema imeendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo pamoja na taasisi zake katika kubuni na kuendeleza mifumo ya kidijitali inayorahisisha utoaji wa huduma, kuongeza uwazi na kuimarisha usimamizi wa shughuli za kilimo nchini.

Akizungumza kwenye Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa e-GA, Bi. Subira Kaswaga, alisema mamlaka hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kuifanya sekta ya kilimo kuwa ya kisasa kupitia matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano.

Alisema miongoni mwa mifumo muhimu iliyojengwa kwa ushirikiano na Wizara ya Kilimo ni mfumo wa M-Kilimo, unaowezesha serikali kupata taarifa za wakulima, kusimamia taasisi zilizo chini ya wizara na kurahisisha utoaji wa vibali mbalimbali vinavyohusiana na shughuli za kilimo.

"Mfumo huu ni dirisha muhimu la usimamizi wa shughuli za kilimo na unasaidia serikali kupata takwimu sahihi pamoja na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma," alisema.

Kaswaga alisema e-GA pia imejenga mfumo wa MUVU kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Vyama vya Ushirika, ambao unasimamia shughuli za vyama vya ushirika kwa njia ya kidijitali.

Alisema mfumo huo unawawezesha wanachama kufuatilia mazao yao kuanzia yanapowasilishwa hadi yanapouzwa, hivyo kuongeza uwazi katika biashara na kuhakikisha wakulima wanapata taarifa sahihi kuhusu mapato yao.

Kwa mujibu wa Kaswaga, zaidi ya vyama vya ushirika 6,000 tayari vimesajiliwa kwenye mfumo huo, hatua ambayo imechangia kupunguza changamoto za upotevu wa mapato na kuimarisha uwajibikaji katika vyama vya ushirika.

Aidha, alisema e-GA imeunda mfumo wa Fertilizer Information System (FIS) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), unaowezesha kusimamia wazalishaji, waagizaji na wasambazaji wa mbolea pamoja na kufuatilia mwenendo wa bei sokoni.

Alisema mfumo huo unaisaidia serikali kuhakikisha wauzaji wa mbolea wanazingatia bei elekezi zinazotolewa na serikali, jambo linalowalinda wakulima dhidi ya ongezeko holela la bei na kuwawezesha kupata pembejeo kwa gharama stahiki.

Mbali na mifumo inayohusiana moja kwa moja na kilimo, Kaswaga alisema taasisi za sekta hiyo zinatumia pia mifumo mingine ya serikali ikiwemo Government Mailing System (GMS) na e-Office, ambayo imeongeza ufanisi wa mawasiliano na utendaji wa kazi serikalini.

Alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wananchi wanaotembelea Maonesho ya Nanenane kutembelea banda la e-GA ili kujionea mifumo mbalimbali ya kidijitali inayotumiwa kuboresha utoaji wa huduma za serikali, hususan katika sekta ya kilimo.