GST YAONGEZA KASI YA UTAFITI WA MADINI KUFANIKISHA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050
DODOMA: Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imeongeza kasi ya utafiti wa kijiosayansi nchini kwa lengo la kuvutia uwekezaji katika sekta ya madini, kuongeza ajira, mapato ya Serikali na kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mkurugenzi Mtendaji wa GST, Eng. Ally Samaje, amesema taasisi hiyo inaendelea kupanua tafiti za jiolojia, kijiofisikia na kijiokemia ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na taarifa sahihi na za kisasa zitakazowawezesha wawekezaji na wachimbaji kufanya maamuzi yenye tija.
Akizungumza katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Eng. Samaje alisema GST ndiyo msingi wa mnyororo mzima wa sekta ya madini kwa kuwa hukusanya, kuchakata, kuhifadhi na kusambaza taarifa muhimu za kijiosayansi kwa wawekezaji na wadau mbalimbali.
Alisema hadi sasa taasisi hiyo imekamilisha utafiti wa jiolojia kwa asilimia 98 ya eneo lote la Tanzania, huku utafiti wa kijiofisikia wa kiwango cha kawaida ukifikia asilimia 100, hatua inayowapa wawekezaji taarifa za awali kuhusu maeneo yenye fursa za madini.
Kwa upande wa utafiti wa kijiofisikia wa kina (High Resolution Airborne Geophysical Survey), alisema umefikia asilimia 16 ya eneo la nchi, lakini maandalizi ya kuongeza kiwango hicho yanaendelea kupitia programu mpya za urushaji ndege katika maeneo yenye rasilimali nyingi za madini.
Alifafanua kuwa awamu ya kwanza ya programu hiyo itahusisha eneo lenye ukubwa wa asilimia 18 ya nchi, hatua itakayoongeza kiwango cha utafiti huo hadi asilimia 34 baada ya kukamilika, huku mkandarasi wa utekelezaji akiwa tayari amepatikana.
Aidha, alisema awamu inayofuata itafanyika katika maeneo ya katikati ya Tanzania yenye ukubwa wa takribani asilimia 19 ya nchi, jambo litakalowezesha kufikia zaidi ya asilimia 50 ya utafiti wa kijiofisikia wa kina kabla ya mwaka 2030, kulingana na malengo ya Serikali.
Eng. Samaje alisema pia GST imefikia asilimia 24 ya utafiti wa kijiokemia nchini na katika mwaka huu wa fedha itafanya tafiti katika maeneo 18 mapya ili kuongeza kiwango hicho hadi asilimia 30.
Alieleza kuwa maeneo mengi yaliyochaguliwa kwa utafiti yana wachimbaji wadogo wa madini, ambapo taarifa zitakazopatikana zitawawezesha kufanya uchimbaji kwa uhakika badala ya kubahatisha, kuongeza uzalishaji na kuboresha kipato chao.
Aliongeza kuwa taarifa hizo zitawasaidia wachimbaji wadogo kupata mikopo kutoka taasisi za fedha, huku GST ikiwa tayari kuthibitisha matokeo ya tafiti zake ili kuongeza imani ya wakopeshaji.
Kwa mujibu wa Eng. Samaje, utekelezaji wa programu hizo unawezeshwa na Mfuko wa Utafiti wa Madini unaotokana na fedha za retention zinazokusanywa kupitia sekta ya madini.
Alisema upatikanaji wa taarifa sahihi za kijiosayansi utapunguza hatari kwa wawekezaji, kuongeza uwekezaji katika utafiti na uchimbaji wa madini, kuchochea uanzishaji wa migodi mipya, kuimarisha viwanda vinavyotumia madini kama malighafi na kuongeza mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.




