UDSM YAONYESHA TAFITI ZA NYUKI NA UBUNIFU WA TEKNOLOJIA YA KILIMO NANENANE
DODOMA: Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kupitia Ndaki ya Sayansi ya Kilimo na Teknolojia ya Chakula, kimesema tafiti zake kuhusu nyuki, hususan nyuki wasiodunga, pamoja na ubunifu wa teknolojia za kisasa za kilimo, zina mchango mkubwa katika kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza uzalishaji wa mazao na kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Akizungumza katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Mwanasayansi wa Nyuki kutoka UDSM, Gabriel Mwambogela, alisema zaidi ya asilimia 75 ya mimea ya chakula hutegemea uchavushaji unaofanywa na nyuki, hivyo kuwafanya kuwa wadudu muhimu katika kuongeza uzalishaji wa kilimo.
Alisema tafiti zilizofanywa na chuo zimebaini kuwa Tanzania ina takribani aina 12 za nyuki wasiodunga, ambapo baadhi wanapatikana katika maeneo yote ya nchi na wengine hupatikana katika maeneo maalumu. Aidha, alisema tafiti za maabara zimeonesha kuwa asali ya nyuki hao ina uwezo wa kupambana na bakteria na fangasi pamoja na kusaidia kutibu vidonda.
Mwambogela alisema UDSM pia imebuni mizinga maalumu inayowawezesha wananchi kufuga nyuki wasiodunga kwa urahisi katika maeneo mbalimbali ikiwemo majumbani na mashuleni, kutokana na tabia yao ya kutokuwa na madhara kwa binadamu.
Aliongeza kuwa ufugaji wa nyuki hao ni fursa ya kiuchumi kwani lita moja ya asali yake huuzwa kati ya Shilingi 50,000 na 70,000, huku akisisitiza kuwa utunzaji wa nyuki unachangia kuongeza mavuno kupitia uchavushaji bora na kuunga mkono jitihada za kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050
Katika maonesho hayo, wanafunzi wa mwaka wa tatu wa programu ya Sayansi na Teknolojia ya Ufugaji Nyuki walionesha bidhaa mbalimbali walizobuni kutokana na mazao ya nyuki, zikiwemo dawa ya asili ya kikohozi, dawa ya kung'arisha viatu, sabuni za kuogea na za kunawia mikono.
Walisema bidhaa hizo zinatumia malighafi za asili, ni salama kwa afya na mazingira, huku dawa ya kikohozi iliyotengenezwa kwa asali ya nyuki wasiodunga na mimea tiba ikitoa mbadala wa bidhaa zenye kemikali nyingi ambazo zinaweza kusababisha mzio kwa baadhi ya watumiaji.
Aidha, wanafunzi wengine walionesha mbolea na viuatilifu vya asili vinavyosaidia kuongeza ukuaji wa mimea na kupunguza magonjwa ya fangasi kwenye mbegu, wakisema matumizi yake yanaweza kupunguza utegemezi wa kemikali mashambani na kuhifadhi mazingira.
Katika upande wa teknolojia ya kilimo, mwanafunzi wa Teknolojia ya Kilimo aliwasilisha mfumo wa Smart Farm unaotumia taarifa za udongo na hatua za ukuaji wa mimea kupima kiwango sahihi cha maji kinachohitajika shambani. Alisema ubunifu huo unalenga kuwasaidia wakulima kutumia maji kwa ufanisi, kuongeza uzalishaji wa mazao na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.





