POSTA KUBORESHA HUDUMA KUENDANA NA MAHITAJI YA WANANCHI
Na Mwandishi Wetu - SHIRIKA la Posta Tanzania limesema litaendelea kuboresha huduma zake ili kuendana na mabadiliko ya mahitaji ya wananchi na kuhakikisha huduma za mawasiliano na usafirishaji zinawafikia watu wengi zaidi nchini.
Akizungumza baada ya kutolewa kwa ripoti ya hali ya sekta ya mawasiliano, Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo wa Shirika la Posta Tanzania, Ferdinand Kabiyemela, aliyemwakilisha Postamasta Mkuu, amesema ripoti hiyo inaonyesha ukuaji wa sekta ya mawasiliano na kuongezeka kwa matumizi ya huduma hizo.
Kabiyemela amesema ongezeko la takwimu katika sekta hiyo linaashiria kuwa huduma za mawasiliano zinazidi kuwafikia wananchi na kueleweka, jambo linalosaidia kuwezesha shughuli za kiuchumi, afya na elimu.
Amesema kwa upande wa Shirika la Posta Tanzania, matokeo hayo ni chachu ya kuendelea kuboresha huduma zake, ikiwemo usafirishaji wa vifurushi, nyaraka, mizigo na vipeto ndani na nje ya nchi.
“Mahitaji ya watumiaji yanabadilika kila siku, hivyo marekebisho bado yanahitajika ili kuhakikisha huduma zinakuwa bora zaidi na zinawafikia watu wengi zaidi,” amesema Kabiyemela.
Amesema Shirika la Posta Tanzania lina mtandao mpana unaofika katika takribani kila wilaya na halmashauri nchini, huku likiwa na uwepo pia Zanzibar na visiwani.
Kwa mujibu wa Kabiyemela, shirika hilo linaendelea kuhakikisha huduma zake zinafika mbali zaidi na kukidhi matarajio ya wananchi katika shughuli mbalimbali, ikiwemo elimu, afya na uchumi.
Ameongeza kuwa, pamoja na maendeleo yanayoendelea katika huduma za mawasiliano, ikiwemo intaneti na huduma za sauti, bado kuna umuhimu wa kuendelea kufanya maboresho ili kuongeza ufanisi na kuwafikia watumiaji wengi zaidi.




