Breaking News

TTCL YAONGOZA UBORA WA HUDUMA ZA MAWASILIANO KWA ASILIMIA 98

Na Mwandishi Wetu - SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeongoza katika utoaji wa huduma bora za mawasiliano kwa kufikisha kiwango cha ubora wa huduma (Quality of Service) cha asilimia 98, kwa mujibu wa ripoti iliyowasilishwa na Waziri wa Mawasiliano.

Akizungumza kuhusu ripoti hiyo, Meneja Mahusiano wa TTCL, Esther Mbanguka, amesema shirika hilo limefarijika na kujivunia matokeo hayo, akieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na maboresho makubwa yaliyofanyika katika miundombinu na mifumo ya kuhudumia wateja.

Amesema TTCL imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano pamoja na mifumo ya ndani na nje inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wateja na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma.

“TTCL imekuwa kinara katika utoaji wa huduma bora za mawasiliano. Haya yote yanawezekana kutokana na miundombinu ambayo tumeiboresha zaidi, lakini pia uwekezaji katika mifumo ya ndani na mifumo ya nje ya namna ya kuwahudumia wateja wetu kwa urahisi na unafuu zaidi,” amesema Mbanguka.

Amesema TTCL itaendelea kuboresha miundombinu yake ili huduma za mawasiliano ziwafikie wananchi katika maeneo mbalimbali nchini, sambamba na kuimarisha mifumo ya huduma kwa wateja.

Mbanguka ameongeza kuwa maboresho hayo yataendelea kufanyika kwa kuhakikisha mifumo ya kusaidia utoaji wa huduma inawekwa na kukamilishwa kwa wakati, lengo likiwa ni kuendelea kutoa huduma bora na zenye ufanisi kwa wateja.