HISTORIA KUANDIKWA LEO, RAIS SAMIA KUZINDUA BWAWA LA JULIUS NYERERE
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Agosti 22, 2026, anazindua rasmi Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115, hatua inayotarajiwa kuongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini.
Uzinduzi huo unafanyika baada ya kukamilika kwa mitambo yote tisa ya mradi huo, ambao unalenga kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi, viwanda, biashara na shughuli nyingine za kiuchumi.
Mradi huo umegharimu takribani Shilingi trilioni 7.452 na umefadhiliwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati yenye lengo la kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa.
Kukamilika kwa Bwawa la Julius Nyerere kunatarajiwa kuongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika na kuweka mazingira bora kwa ukuaji wa viwanda, uwekezaji na shughuli mbalimbali za uzalishaji zinazohitaji umeme wa kutosha.
Aidha, mradi huo unatajwa kuwa sehemu muhimu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kuifanya sekta ya nishati kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi, maendeleo ya viwanda, uwekezaji, ubunifu na ustawi wa wananchi.
Uzinduzi wa leo unafunga rasmi safari ya utekelezaji wa moja ya miradi mikubwa ya kimkakati ya Tanzania katika sekta ya nishati.






