Breaking News

TMA YATOA TAHADHARI YA MAFURIKO, MVUA KUBWA MSIMU WA VULI 2026

Dae Es Salaam: Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetabiri mvua za msimu wa Vuli 2026 kuwa za Juu ya Wastani hadi Wastani katika maeneo mengi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka, huku ikionya uwezekano wa kutokea kwa mafuriko, maporomoko ya ardhi na magonjwa ya mlipuko kutokana na ongezeko la mvua.

Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema msimu huo unatarajiwa kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na hali ya El Niño yenye nguvu kubwa.

Kwa mujibu wa mwelekeo huo, mvua zinatarajiwa kuongezeka zaidi mwezi Novemba 2026, huku mvua za nje ya msimu zikitabiriwa kuendelea hadi Januari 2027, licha ya msimu wa Vuli kwa kawaida kumalizika Desemba.

Maeneo yatakayopata mvua

TMA imesema mvua za Juu ya Wastani hadi Wastani zinatarajiwa katika Kanda ya Ziwa Victoria, Pwani ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki pamoja na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.

Kanda ya Ziwa Victoria, inayojumuisha mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara, pamoja na wilaya za Kakonko na Kibondo mkoani Kigoma, inatarajiwa kuanza kupata mvua kati ya wiki ya nne ya Septemba na wiki ya kwanza ya Oktoba 2026.

Katika Pwani ya Kaskazini, mvua hizo zinatarajiwa kuathiri Dar es Salaam, Tanga, Pwani, kaskazini mwa Morogoro, Mafia pamoja na Unguja na Pemba, na zinatarajiwa kuanza katika wiki ya kwanza na ya pili ya Oktoba.

Kwa upande wa Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, zinazojumuisha Arusha, Manyara na Kilimanjaro, mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya kwanza na ya pili ya Oktoba.

TMA imeonya pia kuwa kutokana na uwepo wa El Niño, baadhi ya maeneo yanaweza kupata vipindi vya mvua mapema mwezi Septemba, ingawa msimu rasmi wa Vuli unatarajiwa kuanza Oktoba katika maeneo mengi.

Mafuriko na athari kwa kilimo

TMA imesema mvua nyingi zinaweza kusababisha unyevu kupita kiasi kwenye udongo na mafuriko, hali inayoweza kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo.

Magonjwa ya mazao yanayosababishwa na kuvu, bakteria na virusi yanaweza pia kuongezeka na kuathiri mazao yakiwemo viazi mviringo, alizeti, maharage, ufuta, matunda na mbogamboga.

Wakulima wametakiwa kuandaa mashamba, kupanda na kutumia pembejeo kwa wakati, huku wakishauriwa kutumia mbinu za kuzuia maji kutuama, mmomonyoko wa udongo na upotevu wa rutuba.
Wafugaji na wavuvi kupewa tahadhari

Kwa wafugaji, ongezeko la mvua linaweza kuongeza upatikanaji wa malisho na maji, lakini TMA imeonya kuhusu uwezekano wa kuongezeka kwa magonjwa ya mifugo, ikiwemo homa ya bonde la ufa na kuoza kwa kwato.

Wakulima wa mwani wameonywa kuhusu athari za kupungua kwa chumvi kwenye maji ya bahari kutokana na mvua nyingi, hali inayoweza kupunguza uzalishaji wa mwani.

Usafiri na ujenzi

TMA imesema mvua kubwa zinaweza kuathiri miundombinu ya barabara, reli, madaraja, bandari na viwanja vya ndege kutokana na mafuriko na mmomonyoko wa udongo.

Miundombinu ya reli za MGR na SGR inaweza pia kuathirika, huku shughuli za upakiaji na upakuaji mizigo bandarini zikitarajiwa kukumbwa na ucheleweshaji katika baadhi ya maeneo.

Sekta ya ujenzi imetakiwa kuzingatia utabiri huo katika kupanga shughuli zake, huku wakandarasi wakishauriwa kuhamisha mitambo na vifaa kutoka maeneo ya mabonde na kuhifadhi vifaa vinavyoharibiwa na unyevu, kama saruji na nondo, katika maeneo salama.

Miji yatakiwa kujiandaa

Mamlaka za Serikali za Mitaa zimetakiwa kuboresha mifumo ya mifereji ya maji na kuimarisha kamati za maafa katika ngazi za mikoa, wilaya, kata, vijiji na mitaa ili kukabiliana na athari za mafuriko.

TMA pia imeshauri mamlaka za afya kujiandaa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko yanayoweza kusababishwa na uchafuzi wa maji, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.

TMA yawataka wanahabari kutumia taarifa rasmi

TMA imewataka waandishi wa habari kutumia na kusambaza taarifa rasmi za hali ya hewa zinazotolewa na mamlaka hiyo pekee, ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kwa wakati.

Kwa mujibu wa TMA, waandishi wanapaswa pia kupata mwongozo wa kitaalamu kutoka kwa wataalamu wa hali ya hewa na sekta husika na kuwasilisha taarifa hizo kwa lugha rahisi na inayoeleweka kwa umma.

TMA imesema itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa taarifa za utabiri wa saa 24, siku 10, mwezi pamoja na tahadhari kulingana na mahitaji.

Mamlaka hiyo imewahimiza wananchi na wadau katika sekta mbalimbali kuendelea kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa na kuchukua hatua za mapema kulingana na ushauri wa wataalamu.