SERIKALI YAITAKA TADB IONGEZE UWEZO WA KIFEDHA KUCHOCHEA MAPINDUZI YA KILIMO
Dodoma - Serikali imeiagiza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kuongeza uwezo wake wa kifedha ili iweze kufadhili kwa kiwango kikubwa zaidi sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Agizo hilo limetolewa na Waziri Mkuu alipotembelea banda la TADB katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea mkoani Dodoma.
Alisema TADB imeendelea kuwa chombo muhimu cha Serikali katika kuwawezesha wakulima, wafugaji, wavuvi na wawekezaji kwa kuwapatia mitaji ya kuendesha shughuli za uzalishaji.
Waziri Mkuu alisema mafanikio ya azma ya Serikali ya kuongeza tija katika sekta ya kilimo yanategemea kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa mitaji ya kutosha, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuiongezea benki hiyo uwezo ili ikidhi mahitaji yanayoongezeka ya wadau wa sekta hizo.
Alisisitiza kuwa Serikali haiwezi kutegemea ruzuku pekee katika kuendeleza kilimo, bali taasisi za kifedha zinapaswa kuwa nguzo muhimu ya uwekezaji kwa kuhakikisha wakulima, wafugaji na wavuvi wanapata mikopo kwa wakati na kwa masharti yanayowawezesha kuongeza uzalishaji.
Aidha, aliitaka TADB kuongeza ufadhili wa ununuzi wa mbolea, pembejeo, zana za kisasa za kilimo pamoja na miradi ya kuongeza thamani ya mazao, ili kuboresha ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Pia aliiagiza benki hiyo kushirikiana na Wizara za Kilimo na Mifugo pamoja na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuwekeza katika miundombinu ya baada ya mavuno, hususan ujenzi wa maghala ya kuhifadhi mazao, hatua itakayowawezesha wakulima kutumia mazao yao kama dhamana kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Frank Nyabundege, alisema benki hiyo imeendelea kufadhili miradi ya kimkakati inayochochea maendeleo ya sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
Alisema TADB tayari imetoa zaidi ya Sh bilioni 700 kwa ajili ya miradi ya umwagiliaji, huku pia ikisaidia maendeleo ya zao la kahawa kupitia vyama vya ushirika katika mikoa ya Kagera na Kigoma.
Nyabundege aliongeza kuwa benki hiyo imefadhili mradi wa kisasa wa ufugaji na uchakataji wa samaki uliopo Bagamoyo, unaotumia teknolojia kutoka Misri, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza tija na thamani katika sekta ya uvuvi.




