Breaking News

TRA YAWAKARIBISHA WANANCHI KUPATA HUDUMA ZA KODI NA TIN NANE NANE DODOMA

Dodoma - Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema ushiriki wake katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nane Nane yanayoendelea kitaifa mkoani Dodoma unalenga kuwafikishia wananchi huduma mbalimbali za kodi pamoja na elimu itakayowasaidia wakulima, wafugaji, wavuvi na wafanyabiashara kutimiza wajibu wao wa kikodi kwa urahisi.

Akizungumza katika maonesho hayo, Afisa Mwandamizi wa Kodi wa TRA, Jackline Ntare, alisema taasisi hiyo inatoa huduma mbalimbali zikiwemo usajili wa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN), makadirio ya kodi, elimu kuhusu mfumo wa iDRAS pamoja na huduma nyingine za kidijitali zinazorahisisha ulipaji wa kodi.

Alisema wananchi wanaofika katika banda la TRA na ambao hawana TIN wanapatiwa huduma hiyo papo hapo sambamba na kufanyiwa makadirio ya kodi pale inapohitajika.

Aidha, alisema TRA imewaweka mawakala wa mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFD) kwa ajili ya kuwahudumia wafanyabiashara wanaohitaji mashine hizo, huku pia ikitoa elimu kuhusu matumizi ya mfumo wa Electronic Tax Stamps (ETS) kwa ajili ya kuhakiki vinywaji na stempu za kielektroniki.

Ntare aliongeza kuwa mamlaka hiyo inaendelea kutoa elimu kuhusu vivutio na misamaha ya kodi inayotolewa na Serikali kwa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuchochea ukuaji wa sekta hizo.

Aliwataka wananchi kutembelea banda la TRA lililopo ndani ya jengo la Taasisi za Fedha katika maonesho hayo ili kupata huduma na elimu mbalimbali za kodi kabla ya maonesho hayo kufungwa Agosti 8.
Kwa upande wake, mkazi wa Dodoma, Shabani Pazi, alisema amefanikiwa kupata huduma ya TIN baada ya kukumbana na changamoto za kimfumo alipokuwa akiomba huduma hiyo.

Alisema alipofika katika banda la TRA alipokelewa na kuhudumiwa kwa muda mfupi, hali iliyomwezesha kupata TIN aliyokuwa akiihitaji bila usumbufu.

Pazi aliwahimiza wananchi wengine wenye uhitaji wa huduma mbalimbali za TRA kutumia fursa ya maonesho ya Nane Nane kufika katika banda la mamlaka hiyo ili kupata huduma kwa haraka na kwa ufanisi.