Breaking News

TTCL KUENDELEA NA OFA ZA VIFAA VYA INTANETI BAADA YA NANENANE

Na Mwandishi Wetu, Dodoma - SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeeleza kuwa ofa ya vifaa vya intaneti iliyokuwa ikitolewa wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima ya Nane Nane itaendelea hata baada ya maonesho hayo kumalizika.

Akizungumza jijini Dodoma baada ya kufungwa kwa maonesho hayo yaliyofanyika katika Viwanja vya John Malecela, Nzuguni, Afisa Mahusiano Mwandamizi wa TTCL, Debora Ngalima, amesema wananchi wataendelea kupata huduma hizo kupitia vituo vya shirika hilo vilivyopo maeneo mbalimbali nchini.

Amesema maonesho hayo yamekuwa pia fursa kwa wananchi kutembelea banda la TTCL na kupata taarifa kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na shirika hilo.

“Tunawashukuru wananchi wote kwa kutembelea banda letu katika maonesho haya ya Nane Nane. Pamoja na maonesho kufikia tamati, ofa katika vifaa vya intaneti itaendelea kama kawaida,” amesema Ngalima.

Ameongeza kuwa huduma za TTCL zitaendelea kupatikana katika vituo na maduka ya shirika hilo yaliyopo sehemu mbalimbali nchini.