Breaking News

TUME YA UMWAGILIAJI YAZINDUA MPANGO WA AJIRA KWA VIJANA, YAGAWA PAMPU 2,000 KWA WAKULIMA

Dodoma. Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imesema katika mwaka wa fedha 2026/27 itazindua zaidi ya miradi 30 ya umwagiliaji, kugawa pampu zaidi ya 2,000 kwa wakulima na kutekeleza mpango wa uchimbaji wa visima utakaotoa ajira kwa kati ya vijana 2,000 na 4,000 nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 32 ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Raymond Mndolwa, alisema hatua hizo ni sehemu ya mkakati wa kuongeza uzalishaji wa kilimo kupitia umwagiliaji na kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Alisema Tume inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya umwagiliaji ambapo makandarasi 146 tayari wanaendelea na kazi katika maeneo tofauti, huku miradi 634 ikiwa katika hatua ya usanifu.

"Tunatarajia kuzindua zaidi ya miradi 30 katika mwaka huu wa fedha 2026/27 ili kuongeza maeneo yanayopata huduma za umwagiliaji na kuinua uzalishaji wa kilimo," alisema Mndolwa.

Aidha, alisema Tume imeanza mpango wa kugawa pampu 1,000 za kutumia maji ya mito na mabonde (surface pumps) katika mikoa saba, ambapo zoezi hilo litaanza mkoani Katavi Agosti 11 mwaka huu.

Alisema pampu hizo zitawawezesha wakulima kupata maji kwa ajili ya umwagiliaji bila kuharibu mazingira, hivyo kuongeza uzalishaji wa mboga mboga na matunda.

Mbali na hilo, Mndolwa alisema Tume imenunua pia pampu zaidi ya 1,000 zinazotumia nishati ya jua (solar pumps), ambazo zitagawiwa wakulima wa parachichi waliopo nje ya maeneo ya kawaida ya miradi ya umwagiliaji ili kuwasaidia kupata maji kwa urahisi.

Kuhusu mpango wa uchimbaji wa visima, alisema hadi sasa visima 415 vimekwishachimbwa, huku zoezi hilo likiendelea katika mikoa na wilaya nyingine nchini.

Alisema mradi huo umebuniwa pia kuwa chanzo cha ajira kwa vijana wenye taaluma za uhandisi na ufundi, ambao wataunda vikundi vitakavyosimamia uchimbaji na ufungaji wa miundombinu ya visima katika halmashauri 184 nchini.

"Ndani ya miaka mitatu tunatarajia sekta hii kuajiri kati ya vijana 2,000 na 4,000. Hii ni sehemu ya juhudi za Serikali kuwawezesha vijana kujiajiri kupitia shughuli za uzalishaji badala ya kutegemea ajira za kawaida," alisema.

Mndolwa alisema Tume imeweka lengo la kuchimba visima 67,000 ifikapo mwaka 2035 na kuwataka vijana kujitokeza kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mpango huo utakaotekelezwa katika halmashauri zote nchini.