Breaking News

WAKULIMA WAHIMIZWA KUITUMIA OFISI YA MSULUHISHI WA MIGOGORO YA BIMA KUDAI HAKI ZAO KUPITIA

Dodoma - Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima imewataka wananchi, hususan wakulima waliokata bima kupitia benki au mawakala wa bima, kufahamu haki zao na kutumia chombo hicho kutatua migogoro ya fidia badala ya kukimbilia mahakamani.

Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Msuluhishi Mkuu wa Migogoro ya Bima, Aloyce Mbunito, alisema ofisi hiyo iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria Sura ya 394 ina jukumu la kutatua migogoro ya bima kwa njia mbadala wa mahakama, kulinda watumiaji wa huduma za bima na kuongeza imani ya wananchi katika sekta hiyo.

Mbunito alisema migogoro inayopokelewa mara nyingi ni pamoja na kukataliwa kwa madai ya fidia, kulipwa fidia isiyolingana na hasara halisi, kucheleweshwa kwa majibu ya madai pamoja na kutokuelewana kuhusu tafsiri ya mikataba ya bima.

Alisema tangu ofisi hiyo ianze kazi mwaka 2025 imefanikiwa kutatua zaidi ya migogoro 2,015, jambo linaloonyesha kuwa wananchi wengi wameanza kutambua umuhimu wa kuitumia kupata haki zao wanapokumbana na changamoto za bima.

Aidha, alieleza kuwa katika maonesho hayo walitembelewa na viongozi wa vyama vya ushirika vya wakulima kutoka mkoani Mara waliowasilisha changamoto za wakulima wa tumbaku waliopata hasara kutokana na mvua ya mawe licha ya kuwa walikuwa wamekata bima kupitia benki.

Kwa mujibu wa Mbunito, changamoto kubwa iliyobainika ni baadhi ya wakulima kutokujua kampuni za bima zilizowahudumia kwa kuwa walikata bima kupitia benki zilizokuwa mawakala wa bima, huku wengi wakikosa mikataba ya bima ambayo ni nyaraka muhimu katika kufuatilia madai yao.

Naye Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mara WAMACU, Momanyi Range, alisema elimu waliyoipata katika banda la Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima imewafungua macho kuhusu umuhimu wa kuwa na mikataba ya bima na kuhifadhi ushahidi wa majanga, ikiwemo kupiga picha za mazao yaliyoharibiwa ili kurahisisha madai ya fidia.

Alisema chama hicho sasa kitawaongoza wakulima wote walioathiriwa kukusanya malalamiko yao, kupata mikataba kutoka benki husika na kuyawasilisha katika Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima ili kuhakikisha wanapata haki zao na kuendelea na shughuli za uzalishaji bila kuathiriwa na hasara za majanga.