Breaking News

BUMAKO INSURANCE YATOA BIMA ZA MOTO NA MIKOPO KWA VYAMA VYA USHIRIKA

DODOMA: Kampuni ya Bumako Insurance imesema inaendelea kutoa huduma mbalimbali za bima kwa vyama vya ushirika nchini, zikiwemo bima ya moto kwa mazao yaliyohifadhiwa maghalani na bima ya mikopo kwa wanachama wa SACCOS, ikiwa ni sehemu ya kulinda mali na kupunguza athari za kifedha zinazosababishwa na majanga.

Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea kitaifa mkoani Dodoma, Mhasibu wa Tawi la Dodoma wa Bumako Insurance, Modest Limo, alisema kampuni hiyo inahudumia vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) na SACCOS kwa kutoa bidhaa mbalimbali za bima zinazokidhi mahitaji yao.

Alisema kupitia bima ya moto, kampuni hiyo hutoa kinga kwa mazao yanayohifadhiwa kwenye maghala, ambapo endapo janga la moto litatokea, wanachama hulipwa fidia kulingana na masharti ya bima.

"Vyama vya ushirika vinajihusisha na shughuli za kilimo, hivyo mazao yanapohifadhiwa maghalani yanaweza kukumbwa na majanga kama moto. Kupitia bima yetu ya fire insurance tunalinda mali hizo na kutoa fidia endapo hasara itatokea," alisema.

Limo aliongeza kuwa Bumako Insurance pia hutoa bima ya mikopo kwa wanachama wa SACCOS, ambayo hulinda mkopaji na taasisi ya kifedha iwapo mkopaji atafariki dunia au kupata ajali itakayomfanya ashindwe kuendelea kurejesha mkopo.

Alisema katika mazingira hayo kampuni hulipa deni lililosalia, hivyo kuondoa mzigo kwa familia ya mkopaji na kuilinda SACCOS dhidi ya hasara inayoweza kujitokeza.

Aidha, alisema Bumako Insurance ni kampuni ya kizalendo yenye uzoefu wa zaidi ya miaka 45 nchini Tanzania, ikiwa na matawi zaidi ya 13 yakiwemo ya Zanzibar.

Aliwahimiza wananchi, vyama vya ushirika na taasisi mbalimbali kutembelea banda la Bumako Insurance katika Maonesho ya Nanenane au kufika katika ofisi za kampuni hiyo zilizopo eneo la Chakwenco, karibu na mataa ya Uwanja wa Ndege wa Dodoma, ili kupata huduma mbalimbali za bima