Breaking News

SANGU AIPONGEZA GGM KWA UWEKEZAJI NA AJIRA

GEITA: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu–Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, ameipongeza Kampuni ya Geita Gold Mining (GGM) kwa uwekezaji katika teknolojia ya uchimbaji madini na hatua inazochukua katika kulinda haki, usalama na maslahi ya wafanyakazi.

Sangu ametoa kauli hiyo Septemba 24, 2026, wakati akitembelea banda la GGM katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Kitaifa yanayofanyika mkoani Geita, akisema kampuni hiyo imeonyesha dhamira ya kutumia teknolojia katika kuboresha shughuli za uchimbaji madini.

Amesema GGM imekuwa mshirika muhimu katika sekta ya ajira na hifadhi ya jamii kwa kutoa ajira kwa Watanzania, huku akisisitiza umuhimu wa kampuni kuhakikisha sheria za kazi zinafuatwa, mazingira ya kazi yanakuwa salama na yenye afya, pamoja na michango ya wafanyakazi kuwasilishwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.

“Niwapongeze sana kwa uwekezaji mkubwa mlioufanya kwenye maonyesho haya. Mmeonyesha hamjaja kushiriki tu, bali mmetaka kuonyesha umma wa Watanzania namna mnavyotumia teknolojia katika kuendesha shughuli zenu za uchimbaji madini,” amesema Sangu.

Aidha, Sangu ameipongeza GGM kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha upatikanaji wa haki za wafanyakazi kupitia ufadhili wa ujenzi wa ofisi za Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), akisema mradi huo umefikia hatua za mwisho.

Amesema hatua hiyo inaonyesha kuwa kampuni hiyo haijazingatia masuala ya uzalishaji na ajira pekee, bali pia imekuwa ikishiriki katika kuwezesha wafanyakazi kupata haki zao kupitia mifumo ya kisheria ya utatuzi wa migogoro ya kazi.

Katika hatua nyingine, Waziri Sangu ameipongeza GGM kwa utekelezaji wa hatua za afya na usalama mahali pa kazi, akibainisha kuwa kampuni hiyo ilipata tuzo katika kikao kilichopita cha Afya na Usalama Mahali pa Kazi kilichofanyika Mbeya.

Amesema Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu–Kazi, Ajira na Mahusiano itaendelea kushirikiana na GGM na wadau wengine wa sekta ya madini kuhakikisha viwango vya kazi vinafuatwa na wafanyakazi wanalindwa.

Sangu pia amempongeza Mbunge wa Kahama Mjini, Mhandisi Chacha, kwa kuendelea kushiriki katika shughuli za sekta ya madini, akibainisha kuwa amekuwa mmoja wa wadau walioshiriki katika maandalizi ya maonesho hayo tangu kuanzishwa kwake.

Amesema sekta ya madini ni muhimu kwa uchumi wa Tanzania kutokana na mchango wake katika uzalishaji na utoaji wa ajira, hivyo Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji na wadau ili sekta hiyo ikue sambamba na maslahi ya wafanyakazi na wananchi.

Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Kitaifa yanafanyika mkoani Geita chini ya kaulimbiu “Madini ni Utajiri, Tuwajibike kwa Pamoja Kufikia Dira ya Taifa 2050.”