Breaking News

BRELA: VIJANA RASIMISHENI VIKUNDI KUNUFAIKA NA FURSA ZA KIUCHUMI

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umewahimiza wanafunzi na wahitimu wa Vyuo Vikuu Nchini kuanzisha, kujiunga na kurasimisha vikundi vyao vya ujasiriamali ili kuongeza uwezo wa kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo mikopo, zabuni na huduma nyingine zinazolenga kuwawezesha vijana.

Wito huo umetolewa leo, Septemba 17, 2026, jijini Dar es Salaam na Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, alipokuwa akitoa wasilisho maalum katika Kongamano la CEO Mindset 2026 lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kufanyika katika Ukumbi wa Confucius Institute wa Chuo hapo.

Kongamano hilo lililenga kuwaandaa wanafunzi na wahitimu wapya kuwa viongozi na wasimamizi wenye uwezo wa kuanzisha na kuendesha taasisi, kampuni na biashara zao kwa ufanisi iliwakutanisha wanafunzi 33 kutoka Ndaki ya Biashara (UDBS), Ndaki ya Elimu (UDSOE), pamoja na Ndaki ya Kilimo na Sayansi ya Chakula (CoAF).

Akizungumza katika kongamano hilo, Bw. Nyaisa alisema urasimishaji wa vikundi ni hatua muhimu kwa vijana wanaotaka kujenga biashara endelevu na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi badala ya vijana kufanya shughuli zao mmoja mmoja, kuunda na kurasimisha vikundi kunaweza kuwawezesha kuwa na nguvu ya pamoja katika kutafuta mitaji, fursa za biashara pamoja na zabuni mbalimbali zinazotolewa na Serikali.

"Vijana mnapaswa kuanza kufikiria zaidi ya mtu mmoja mmoja. Mkiwa katika vikundi vilivyorasimishwa mnaweza kujenga nguvu ya pamoja na kuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kutafuta fursa za kiuchumi, usajili na urasimishaji wa biashara ni hatua muhimu katika safari ya kijana kutoka kuwa na wazo la biashara hadi kuwa mjasiriamali mwenye shughuli inayotambulika" alisema Bw. Nyaisa