Breaking News

BoT YAHIMIZA MATUMIZI YA MALIPO YA KIDIJITALI

GEITA - Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewahimiza wafanyabiashara, hususan wa sekta ya madini, kutumia mifumo ya malipo ya kidijitali ili kupunguza matumizi ya fedha taslimu, kuongeza kasi ya mzunguko wa fedha na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Akizungumza katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Kitaifa yanayofanyika mkoani Geita, Afisa Msimamizi wa Mifumo ya Malipo nchini kutoka BoT, Fredrick Kimaro, amesema matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali yanaweza kupunguza changamoto zinazohusishwa na matumizi ya fedha taslimu, ikiwemo hatari ya wizi na gharama zinazotokana na usafirishaji wa fedha.

Kimaro amesema BoT imeshiriki maonesho hayo kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mifumo ya malipo na kuwahamasisha kutumia njia salama na za haraka katika kufanya miamala, hatua inayolenga kuendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema njia za malipo zinazoweza kutumiwa na wananchi na wachimbaji wa madini ni pamoja na mobile banking, internet banking, mashine za POS na Lipa Namba, ambazo zinawezesha kufanya na kupokea malipo bila kutegemea fedha taslimu.

Kwa mujibu wa Kimaro, matumizi ya mifumo hiyo yanawezesha malipo kufanyika kwa haraka hata pale mlipaji na mpokeaji wanapokuwa katika maeneo tofauti, hivyo kuongeza kasi ya mzunguko wa fedha katika uchumi.

Aidha, amesema BoT inasimamia mifumo ya malipo nchini ili kuhakikisha inakuwa salama na inalinda watumiaji, huku akiwataka wananchi wenye changamoto za miamala kuwasiliana kwanza na watoa huduma wao.

Amesema endapo mtumiaji hataridhika na huduma au utatuzi uliotolewa na mtoa huduma, anaweza kuwasilisha malalamiko yake Benki Kuu kupitia njia zilizowekwa kwa ajili ya kushughulikia malalamiko ya watumiaji wa huduma za kifedha.

Kimaro ametoa wito kwa wafanyabiashara wa madini na wananchi kwa ujumla kuongeza matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali ili kusaidia kupunguza utegemezi wa fedha taslimu na kuchangia utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050