Breaking News

TPDC YATOA ELIMU YA MAFUTA NA GESI GEITA

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limetumia Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Kitaifa yanayofanyika mkoani Geita kutoa elimu kwa wananchi na wadau kuhusu shughuli zake katika utafiti, uzalishaji, uendelezaji na usambazaji wa mafuta na gesi nchini.

Akizungumza katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Geita, Afisa Masoko wa TPDC, Bi. Grace Chigugu, amesema shirika hilo limeleta teknolojia mbalimbali katika maonesho hayo ili kuwawezesha wananchi kuelewa namna shughuli za mafuta na gesi zinavyotekelezwa.

Amesema teknolojia hizo zinatumika katika hatua mbalimbali, ikiwemo utafiti wa mafuta na gesi kwa kutambua miamba tabaka yenye viashiria vya uwepo wa rasilimali hizo, uchakataji wa gesi asilia na usafirishaji wake hadi kwa mtumiaji wa mwisho.

Chigugu amesema TPDC pia inatumia teknolojia ya Virtual Reality (VR) katika banda lake, inayowawezesha wananchi kujionea kwa njia pepe hatua za uchimbaji, uchakataji na usafirishaji wa gesi asilia.

Amesema ushiriki wa TPDC katika maonesho hayo pia unalenga kuwaeleza wananchi wa Geita kuhusu miradi ya shirika inayowanufaisha, ikiwemo Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), ambao unapita katika mikoa mbalimbali ikiwemo Geita.

Aidha, amesema kampuni tanzu ya TPDC, TANOIL Investments Limited, inamiliki kituo cha mafuta mkoani Geita, kinachotoa fursa kwa wachimbaji na wadau wengine kupata nishati ya mafuta kwa ajili ya shughuli za uzalishaji.

Kwa upande wa gesi asilia, Chigugu amesema TPDC imeanza kusambaza gesi katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Arusha, Kilimanjaro na Tanga katika mwaka huu wa fedha, huku Geita ikitarajiwa kuwa miongoni mwa mikoa itakayofikiwa katika kipindi cha miaka miwili ijayo.

Amewaalika wananchi na wadau wa Geita kutembelea banda la TPDC katika maonesho hayo ili kupata elimu na kufahamu fursa mbalimbali zinazotokana na shughuli za mafuta na gesi nchini.