Breaking News

BRELA YATOA ELIMU YA MILIKI UBUNIFU KWA WAFANYABIASHARA GEITA

GEITA - Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umewataka wafanyabiashara na wabunifu mkoani Geita kusajili alama za biashara na kulinda hati miliki za uvumbuzi wao ili kuimarisha ulinzi wa bidhaa na huduma zao.

Wito huo umetolewa na Afisa Mwandamizi kutoka BRELA, Athumani Salumu Makuka, wakati akizungumza katika banda la BRELA kwenye Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Kitaifa yanayofanyika mkoani Geita.

Makuka amesema BRELA inatumia maonesho hayo kutoa elimu kuhusu usajili wa biashara, makampuni, majina ya biashara, leseni pamoja na miliki bunifu, ikiwemo alama za biashara na hati miliki.

Amesema hati miliki hulinda uvumbuzi mpya unaolenga kutatua changamoto mbalimbali, akitoa mfano wa uwezekano wa vijana wabunifu kubuni mitambo midogo itakayowasaidia wachimbaji wadogo katika shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini.

“Tunawasaidia kuwapa ulinzi wa hati miliki (patent),” amesema Makuka.

Aidha, amesema BRELA inalinda pia alama za biashara zinazotambulisha bidhaa au huduma, huku akiwataka wafanyabiashara kuhakikisha nembo na chapa zao zinasajiliwa ili kuepuka kutumiwa na watu wengine.

Makuka amesema usajili wa alama za biashara umegawanyika katika madaraja 45 kulingana na aina ya bidhaa au huduma, huku akitaja baadhi ya madaraja yanayoweza kuwa muhimu kwa wafanyabiashara wa madini na sekta nyingine.

Amesema wakati wa maonesho hayo wananchi wanaweza kupata elimu na kusaidiwa kufanya usajili wa biashara na miliki bunifu bila kulipia gharama za huduma ya ufuatiliaji au usaidizi, isipokuwa ada zinazotakiwa kulipwa serikalini.

“Ukija hapa utalipa tu pesa ya serikali, lakini kwenye facilitation za kufanya usajili, huduma hiyo inapatikana bure katika muda huu ambao tupo hapa maoneshoni,” amesema.

BRELA imewahimiza wananchi kutumia fursa hiyo kujifunza na kusajili biashara, chapa na ubunifu wao ili kupata ulinzi wa kisheria na kuongeza thamani ya biashara zao.