VETA YAELIMISHA WACHIMBAJI KUHUSU VIATU VYA USALAMA
GEITA - Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imewaelimisha wachimbaji na wadau wa sekta ya madini kuhusu umuhimu wa kutumia viatu maalumu vya usalama wanapotekeleza shughuli zao katika maeneo ya kazi.
Mwalimu wa Bidhaa za Ngozi kutoka Chuo cha VETA Dakawa, Morogoro, Dakawa Hamidu Shabani, amesema hayo wakati akizungumza katika banda la VETA kwenye Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Kitaifa yanayofanyika mkoani Geita.
Amesema VETA imeshiriki maonesho hayo kwa kuonyesha bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa na vyuo vyake, ikiwemo viatu vya usalama vinavyolenga kuwakinga wafanyakazi na wachimbaji dhidi ya madhara yanayoweza kutokea katika maeneo ya kazi.
Kwa mujibu wa Shabani, viatu hivyo vimetengenezwa kwa kuwekwa chuma katika sehemu ya mbele ili kuongeza ulinzi wa miguu na kusaidia watumiaji kutekeleza shughuli zao kwa usalama zaidi.
Amesema maonesho hayo pia yamekuwa fursa kwa VETA kuwaelimisha wananchi kuhusu ujuzi unaotolewa na taasisi hiyo, pamoja na bidhaa zinazoweza kuzalishwa kupitia mafunzo ya ufundi stadi.
“Jana walikuja wachimbaji hapa na kuchukua viatu vyetu vya usalama, wakaenda navyo kwenye semina za OSHA wakiwa wamevaa bidhaa zilizotengenezwa katika Chuo cha VETA Dakawa,” amesema.
Shabani amesema VETA inaendelea kutoa fursa za mafunzo ya ufundi stadi kwa Watanzania katika maeneo mbalimbali nchini, akiwataka wananchi kutumia fursa hizo kujifunza ujuzi utakaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa.
Amesema udahili wa wanafunzi kwa ajili ya mafunzo ya muda mrefu ulianza Agosti mwaka huu na unatarajiwa kukamilika Septemba, huku akisisitiza kuwa VETA inaendelea na kaulimbiu yake ya “Ufundi Stadi, Fursa Kama Zote kwa Watu Wote.”




