Breaking News

GEITA: WAJASIRIAMALI WAHIMIZWA KUSAJILI NEMBO NA MAJINA YA BIASHARA

GEITA - Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umewataka wafanyabiashara, wajasiriamali na wavumbuzi kutumia fursa ya Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Kitaifa yanayoendelea mkoani Geita kupata elimu na huduma za usajili wa biashara, kampuni, majina ya biashara, alama za biashara pamoja na hati miliki.

Rai hiyo imetolewa na Afisa Usajili wa BRELA, Athuman Makuka, wakati akizungumza katika maonesho hayo yanayoendelea mkoani Geita, akisema wananchi wanapaswa kusajili alama zao za biashara, ikiwemo nembo na majina ya bidhaa, ili kulinda haki zao na kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza pale mtu mwingine anaposajili alama hiyo kabla yao.

Makuka amesema BRELA imekuwa ikipokea wananchi wanaohitaji huduma mbalimbali, akieleza kuwa tayari wamehudumia pia mvumbuzi kutoka VETA aliyefika kupata maelekezo kuhusu usajili wa uvumbuzi wake.

Amesema wananchi wanaweza pia kupata elimu kuhusu usajili wa viwanda vidogo, ambapo gharama za usajili huanzia Shilingi 10,000, pamoja na kupata elimu ya namna ya kulinda uvumbuzi na mali zao za kiakili.

“Tunasisitiza wafanyabiashara waendelee kuja kusajili nembo zao kwa sababu kuna kesi ambazo zimetokea ambapo mtu anakuwa na nembo lakini hajaisajili, baadaye anagundua mtu mwingine tayari ameshaisajili,” amesema Makuka.

Aidha, Makuka ametumia fursa hiyo kuwaelimisha wafanyabiashara kuhusu mfumo mpya wa BRELA Online System (BOS) ambao umechukua nafasi ya mfumo wa awali wa BRELA Online Registration System (ORS).

Amesema mfumo wa BOS umeboreshwa ili kurahisisha huduma kwa wateja, ambapo kwa sasa mtu mmoja anatumia NIDA moja kufungua akaunti moja, huku baadhi ya taarifa zinazohitajika kujazwa zikiwa zimepunguzwa ili kuokoa muda.

Kwa mujibu wa Makuka, mfumo huo pia unawawezesha wakurugenzi wote wa kampuni kupata taarifa zao iwapo wamefungua akaunti zao za BRELA, tofauti na mfumo wa awali ambao upatikanaji wa taarifa ulikuwa na changamoto zaidi.

Amesema BRELA imeweka kituo katika maonesho hayo kwa ajili ya kutoa elimu na kuwasaidia wafanyabiashara, wanasheria na wananchi wengine wanaotaka kujifunza namna ya kutumia mfumo huo mpya.

“BRELA ni lango la mafanikio. Kama mtoto anapokuwa mdogo anahitaji cheti cha kuzaliwa, mfanyabiashara na mjasiriamali anahitaji cheti cha BRELA ili aweze kuendelea mbele,” amesema.

Akizungumzia mwitikio wa wananchi, Makuka amesema umekuwa mkubwa na umeendelea kuongezeka kadiri siku za maonesho zinavyosogea, huku akiwataka wananchi kutumia siku zilizobaki kufika katika banda hilo kupata huduma na elimu.
Kwa upande wake, Mhandisi Audiface Tarimo kutoka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), amewataka wananchi wa Geita na maeneo ya jirani kutembelea banda la BRELA na kutumia huduma zinazotolewa.

Tarimo amesema yeye binafsi amefika katika banda hilo na kupata msaada wa kuhuisha jina la biashara alilolisajili mwaka 2002, akilenga kulitumia katika hatua ya usajili wa kampuni.

Amesema huduma aliyoipata imekuwa nzuri na amewashauri Watanzania wenye changamoto zinazofanana na yake kufika katika banda la BRELA ili kupata msaada na maelekezo sahihi.

Maonesho hayo yanaendelea mkoani Geita, ambapo BRELA inaendelea kutoa huduma na elimu kwa wananchi hadi siku ya mwisho ya maonesho.