Breaking News

WACHIMBAJI GEITA WAALIKWA KUSHIRIKI SIKU YA LOCAL CONTENT MAONESHO YA MADINI

GEITA - Wachimbaji na wadau wanaojihusisha na mnyororo wa thamani wa madini wamealikwa kujitokeza kwa wingi katika Siku ya Local Content itakayofanyika Ijumaa, Oktoba 2, 2026, ikiwa ni sehemu ya Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Kitaifa yanayofanyika mkoani Geita.

Wito huo umetolewa na Katibu wa Chama cha Wachimba Madini Mkoa wa Geita na Mjumbe wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Tanzania (FEMATA), Mwisamila Nyabangi Jeremia, ambaye amesema siku hiyo itatoa fursa kwa wachimbaji na watoa huduma kujifunza na kujadili namna Watanzania wanavyoweza kushiriki zaidi katika shughuli za madini.

Nyabangi amesema Siku ya Local Content inalenga kuhamasisha ushirikishwaji wa Watanzania katika rasilimali za madini na shughuli mbalimbali zinazohusiana na sekta hiyo, akiwataka wachimbaji na watoa huduma kufika katika viwanja vya EPZ, viwanja vya Mama Samia Suluhu Hassan, Geita.

Amesema siku hiyo pia itahudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Waziri wa Madini, Anthony Peter Mavunde, ambaye anatarajiwa kushiriki katika semina zinazohusu Local Content.

Aidha, amesema Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Tanzania (FEMATA), John Wambura Bina, atatembelea mabanda ya maonesho hayo, huku mgeni mwingine anayetarajiwa kushiriki akiwa ni Mchungaji Mwamposa, ambaye pia ni mchimbaji wa madini.

Kwa mujibu wa Nyabangi, uwepo wa wadau hao utatoa fursa kwa wachimbaji na watoa huduma kupata elimu, kubadilishana uzoefu na kusikiliza masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya madini na ushiriki wa Watanzania katika mnyororo wa thamani wa madini.

Aidha, Nyabangi amesema sekta ya uchimbaji madini inaendelea kuhamia katika matumizi ya sayansi na teknolojia, akieleza kuwa wachimbaji wa sasa wanazidi kutumia huduma za kitaalamu, ikiwemo upimaji wa sampuli za madini katika maabara, badala ya kutegemea imani zisizo za kisayansi.

Kwa upande wake, Katibu wa TAOMA na Kiongozi wa Wanawake Wachimbaji wa Madini amewataka wanawake wanaojihusisha na mnyororo wa thamani wa madini, hususan waliopo Geita na wale kutoka mikoa mbalimbali, kujitokeza kwa wingi kushiriki katika shughuli za siku hiyo.

Amesema ushiriki wa wanawake ni muhimu katika kuimarisha nafasi yao katika sekta ya madini, huku akiwataka pia kushiriki katika semina ya Local Content na shughuli nyingine zitakazofanyika wakati wa maonesho hayo.

Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Kitaifa yanaendelea mkoani Geita, yakilenga kutoa elimu, kuonesha teknolojia mbalimbali za uchimbaji na kuongeza uelewa wa wadau kuhusu fursa na shughuli zinazohusiana na sekta ya madini.