DC BURA AIPONGEZA WCF, AITAKA KUONGEZA WANACHAMA
GEITA - Mkuu wa Wilaya ya Chato, Louis Bura, ameuomba Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kuongeza juhudi za kuwafikia na kuwaelimisha waajiri na wafanyakazi ili kuongeza idadi ya wanachama na kuimarisha mfuko huo.
Bura ametoa rai hiyo leo, Septemba 29, 2026, mara baada ya kutembelea banda la WCF katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Kitaifa yanayofanyika mkoani Geita.
Amesema Serikali kupitia viongozi wa maeneo ina utayari wa kushirikiana na WCF katika kuwafikia wadau wengi zaidi, akisisitiza kuwa WCF inaweza kutumia viongozi wa serikali za mitaa kuwaunganisha na wananchi na waajiri katika maeneo mbalimbali.
“Ninachotaka ni kupata watu wengi, members wengi kadri inavyowezekana ili mfuko wetu uwe mkubwa.” amesema Bura.
Ameongeza kuwa viongozi wa maeneo wanaweza kusaidia WCF kuitisha mikutano na wananchi na waajiri katika maeneo ambayo wataalamu wa mfuko huo wanahitaji kutoa elimu kuhusu huduma na umuhimu wa kujiunga na mfuko.
Kwa upande wake, Afisa Tathmini na Viatarishi Mahali pa Kazi wa WCF, Silvanus Kuloshe, amesema taasisi hiyo inafanya kazi kwa karibu na migodi mbalimbali nchini, ikiwemo migodi mikubwa na midogo, kwa lengo la kutathmini vihatarishi vinavyoweza kusababisha madhara kwa afya na usalama wa wafanyakazi.
Kuloshe amesema WCF hutumia vifaa maalumu kupima viwango vya vumbi (dust) katika maeneo ya migodi na kutoa ushauri kwa waajiri kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa pale viwango vinapokuwa juu, huku huduma hiyo ikitolewa bila malipo.
Ameeleza pia kuwa WCF hupima mtikisiko wa mwili mzima (whole body vibration) unaosababishwa na matumizi ya mitambo migodini, kwa kuwa mtikisiko mkubwa unaweza kuchangia matatizo ya kiafya kwa wafanyakazi.
Kwa mujibu wa Kuloshe, baadhi ya changamoto zinazohusishwa na vihatarishi hivyo ni pamoja na magonjwa ya mfumo wa misuli na mifupa (musculoskeletal disorders), matatizo ya mgongo na disc bulge, ambayo yamekuwa miongoni mwa sababu za madai ya fidia kwa wafanyakazi.
WCF imeendelea kutumia maonesho hayo kutoa elimu kwa wadau wa sekta ya madini kuhusu umuhimu wa kutambua na kudhibiti vihatarishi mahali pa kazi, pamoja na huduma zinazotolewa na mfuko huo.






