DC CHATO AHIMIZA MATUMIZI YA NISHATI SAFI, AIPONGEZA TANESCO
GEITA - Mkuu wa Wilaya ya Chato, Luis Bura, amewataka wananchi kushirikiana na taasisi zinazohusika na huduma za nishati katika kutoa taarifa na kulinda miundombinu ya umeme, huku akisisitiza matumizi ya nishati safi ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira.
Bura ametoa kauli hiyo leo, Septemba 29, 2026, mara baada ya kutembelea banda la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Kitaifa yanayofanyika mkoani Geita.
Amesema utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya nishati na utunzaji wa miundombinu ya umeme ni muhimu, kwa kuwa wananchi wanaweza kusaidia kutoa taarifa mapema kuhusu changamoto mbalimbali, ikiwemo nguzo za umeme zinazoweza kuanguka au miundombinu iliyo katika hatari.
Aidha, Bura ameipongeza TANESCO kwa kuimarisha huduma kwa wananchi kupitia matumizi ya teknolojia na mifumo ya mawasiliano katika maeneo mbalimbali, akisema hatua hiyo imechangia kupunguza malalamiko ya wananchi na kurahisisha utatuzi wa changamoto za umeme.
Amesema katika baadhi ya maeneo, wananchi wamekuwa wakipata huduma kwa haraka kupitia vikundi vya mawasiliano vinavyowakutanisha watendaji na wananchi, badala ya kulazimika kufika ofisini kufuatilia changamoto zao.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza umuhimu wa matumizi ya nishati safi, akisema matumizi makubwa ya nishati zinazotokana na ukataji wa miti yanaweza kuongeza uharibifu wa mazingira na kuathiri mustakabali wa nchi.
Bura amesema Serikali imekuwa ikihamasisha matumizi ya nishati safi na kuwataka wananchi kutumia fursa zinazotolewa kupitia TANESCO na REA, ikiwemo majiko yanayotumia teknolojia za kisasa, ili kupunguza utegemezi wa nishati chafu.
Kwa upande wake, Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja Mkoa wa Geita, Lucas Swere, amesema wamekuwa wakitoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuhama kutoka matumizi ya nishati chafu kwenda kwenye matumizi ya nishati safi.
Swere amesema TANESCO imekuja na majiko ya aina mbalimbali yanayolenga kurahisisha upishi na kupunguza matumizi ya nishati zinazochafua mazingira.
Amesema miongoni mwa majiko yanayotolewa ni yale yanayotumia mfumo wa pressure cooker pamoja na majiko ya kisasa yanayotumia teknolojia ya induction.
Ameongeza kuwa wananchi wanahimizwa kutembelea banda la TANESCO katika maonesho hayo ili kupata elimu kuhusu matumizi ya nishati safi, namna ya kulinda mazingira na jinsi teknolojia hizo zinavyoweza kurahisisha shughuli za upishi majumbani.
Kwa mujibu wa viongozi hao, matumizi ya nishati safi yanaweza kusaidia kupunguza ukataji wa miti, kulinda mazingira na kuwezesha wananchi kutumia teknolojia zinazorahisisha maisha ya kila siku.





