Breaking News

GST YAWEKA WAZI HUDUMA NA TAFITI ZA KIJEOLOJIA MAONESHO YA MADINI GEITA

GEITA - Taasisi ya Jeolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imesema inatoa huduma mbalimbali za kitaalamu ikiwemo utafiti wa madini, ushauri elekezi, huduma za maabara na uhifadhi wa taarifa za kijeosayansi.

Afisa Masoko wa GST, Jeremia Mgale, amesema hayo katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika kitaifa mkoani Geita, ambapo GST inashiriki kupitia banda la Wizara ya Madini.

Mgale amesema maonesho hayo yanatoa fursa kwa wadau na wananchi kupata elimu kuhusu huduma zinazotolewa na GST, huku wataalamu wa jiolojia na maabara wakiwa katika banda hilo kutoa ushauri kuhusu utafiti wa madini na masuala ya jiolojia.

Amesema GST itaendelea kutoa huduma katika banda hilo kuanzia mwanzo wa maonesho hadi siku ya mwisho, Septemba 3, na kuwataka wananchi na wadau kulitumia banda hilo kupata huduma na elimu mbalimbali.
Kwa upande wake, Mjeolojia wa GST, Andrew Kula Buluba, amesema taasisi hiyo inatumia maonesho hayo kuonesha tafiti mbalimbali za kijeolojia, geokemia na geofizikia zilizofanywa nchini.

Buluba amesema takwimu zinazooneshwa na GST zinaonesha kuwa tafiti za jeolojia zimefikia asilimia 98, geokemia asilimia 24, huku tafiti za geofizikia zenye mwonekano wa chini (low resolution) zikifikia asilimia 100 na zenye mwonekano wa juu (high resolution) asilimia 16.

Ameongeza kuwa GST pia inaratibu na kutoa ushauri kuhusu majanga ya asili ya kijeolojia, yakiwemo maporomoko ya ardhi na milipuko ya volkano, pamoja na namna ya kujikinga na athari zake.