Breaking News

WAKALA WA VIPIMO ASISITIZA MATUMIZI YA MIZANI ILIYOHAKIKIWA KWENYE MADINI

GEITA - Wakala wa Vipimo umewataka wachimbaji, wafanyabiashara na wadau wa sekta ya madini kuhakikisha wanatumia mizani iliyohakikiwa ili kuzuia udanganyifu, kulinda mapato ya Serikali na kuhakikisha wanunuzi na wauzaji wanapata haki katika biashara ya madini.

Akizungumza katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Kitaifa yanayofanyika mkoani Geita, Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Mwanza, Akilim Zuberi, amesema mizani inayotumika kupimia madini inapaswa kuhakikiwa na Wakala wa Vipimo angalau mara moja kwa mwaka kwa mujibu wa sheria.

Amesema matumizi ya mizani isiyokuwa sahihi yanaweza kusababisha hasara kwa wauzaji na wanunuzi, ikiwamo kupunjwa kwa madini yanayouzwa kwa vipimo vya uzito kama karati, huku Serikali nayo ikipoteza mapato yanayotokana na mrabaha na kodi mbalimbali.

Zuberi amesema Wakala pia huhakiki vipimo vingine vinavyotumiwa katika sekta ya madini, ikiwamo mita za maji, mita za umeme na mita tiririka za mafuta, ili kuhakikisha huduma na bidhaa zinazopimwa zinatolewa kwa usahihi.

Amesema Wakala hufanya ukaguzi katika masoko ya madini na maeneo mengine ya biashara kwa lengo la kuhakikisha mizani na vipimo vinavyotumika vinaendana na matakwa ya kisheria na kulinda maslahi ya wadau.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Kagera, Johnstone Japheth, amewataka wananchi wanaonunua gesi za majumbani kuhakikisha wauzaji wanatumia mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo.

Japheth amesema mtumiaji anapaswa kuhakikisha mzani unaotumika kumpimia gesi una stika ya Wakala wa Vipimo inayoonyesha kuwa umekaguliwa, hatua ambayo itasaidia kupunguza malalamiko kuhusu kupungua kwa kiwango cha gesi kwenye mitungi.

Amesema wananchi wanaweza kufika katika banda la Wakala wa Vipimo kwenye maonesho hayo kupata elimu kuhusu matumizi sahihi ya vipimo katika biashara na namna ya kuhakikisha wanapata bidhaa na huduma kwa viwango vinavyostahili.