MASAUNI: MABADILIKO YA TABIANCHI YAGEUZWE KUWA FURSA ZA KIUCHUMI
DAR ES SALAAM: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yusuf Masauni, amesema Tanzania inapaswa kutumia hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kama fursa za uwekezaji, ajira, ubunifu na kukuza uchumi wa kijani.
Masauni amesema mabadiliko ya tabianchi si changamoto ya kimazingira pekee, bali pia ni suala linalogusa maendeleo ya kiuchumi, hivyo Serikali, sekta binafsi na wadau wengine wanapaswa kuangalia namna ya kubadili changamoto hizo kuwa fursa zenye manufaa kwa wananchi.
Akifungua Tanzania Green Summit 2026 jijini Dar es Salaam, yenye kaulimbiu “Turning Climate Action into Opportunity” (Kugeuza Hatua za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kuwa Fursa), alisema hatua hizo zinaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Alisema Tanzania ina fursa kubwa katika maeneo ya nishati safi, kilimo endelevu, utalii endelevu, usimamizi wa taka, uchumi wa bluu, uhifadhi wa mazingira, teknolojia na biashara ya kaboni, ambazo zinaweza kuleta ajira na kuongeza thamani ya kiuchumi.
Masauni alisema Serikali pia imeendelea kuchukua hatua kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya mazingira na tabianchi, huku akipongeza taasisi za fedha zinazoshiriki katika eneo hilo. Alisema CRDB kwa sasa ni miongoni mwa taasisi zilizopewa kibali chini ya Green Climate Fund (GCF), huku Serikali ikilenga kuongeza idadi ya taasisi za Tanzania zitakazopata fursa hiyo.
Aidha, alisema Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji wa Ofisi ya Kikanda ya Santiago Network on Loss and Damage, itakayosaidia kujenga uwezo wa nchi zinazoendelea kukabiliana na athari na hasara zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Alisema Serikali pia imeendelea kuweka mkazo katika kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kijani, akieleza kuwa Tanzania imekuwa mwenyeji wa Kituo cha Afrika cha Vijana cha Mafunzo ya Mabadiliko ya Tabianchi, kinacholenga kuongeza uwezo wa vijana katika uongozi, ubunifu na hatua za kukabiliana na tabianchi.
Kwa upande wa biashara ya kaboni, Masauni alisema Kituo cha Rasilimali za Biashara ya Kaboni chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais kinaendelea kuwezesha utekelezaji wa miradi katika eneo hilo, huku miradi 117 ikiwa imesajiliwa na iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Alisema Tanzania pia inaendelea kuwekeza katika nishati safi ya kupikia, ikiwa na lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Masauni alitaja pia uzalishaji wa umeme kupitia Mradi wa Julius Nyerere Hydropower Project (JNHPP), unaozalisha megawati 2,115, pamoja na matumizi ya umeme katika reli ya kisasa (SGR), uendelezaji wa bandari na hatua za kuongeza matumizi ya magari ya umeme kuwa ni miongoni mwa juhudi zinazounganisha maendeleo ya kiuchumi na uhifadhi wa mazingira.
Alisema rasilimali za madini muhimu kama nikeli, grafiti na lithiamu nazo zinatoa fursa kwa Tanzania kushiriki katika minyororo ya thamani ya teknolojia za kijani, akisisitiza umuhimu wa kufanya hivyo kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira, uongezaji thamani nchini, uhamishaji wa teknolojia na uundaji wa ajira.
Masauni aliwataka vijana wasichukuliwe kama wanufaika wa programu za tabianchi pekee, bali watambuliwe kama wabunifu, watafiti, wajasiriamali na viongozi wa uchumi wa kijani wa sasa na baadaye.
“Hakutakuwa na uchumi wa kijani bila uwezo, utafiti na teknolojia,” alisema, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, vyuo, taasisi za utafiti na sekta binafsi katika kuibua maarifa, teknolojia na fursa za biashara.
Aidha, alizitaka taasisi za fedha na sekta binafsi kuongeza uwekezaji katika miradi ya uchumi wa kijani na kutoa ubunifu wa kifedha kwa ajili ya miradi inayolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Masauni pia aliipongeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na waandaaji na washirika wa Tanzania Green Summit kwa kuandaa jukwaa hilo, akisema mkutano huo haupaswi kuishia katika majadiliano pekee, bali uzalishe ushirikiano, uwekezaji, teknolojia, tafiti na suluhisho zinazotekelezeka katika jamii.
“Tanzania inaweza kujenga uchumi ambao ulinzi wa mazingira, ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na ustawi wa wananchi vinaenda pamoja,” alisema Masauni.
Tanzania Green Summit 2026 washiriki watajadiliana namna ya kugeuza hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kuwa fursa za kiuchumi na kijamii











