Breaking News

RC CHALAMILA AKAGUA DAMPO - PUGU

DAR ES SALAAM: Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameagiza kuanza kwa mchakato wa kuchakata taka katika Dampo la Pugu kwa kushirikisha sekta binafsi, hatua inayolenga kupunguza mrundikano wa taka na kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo mbolea na gesi.

Chalamila ametoa agizo hilo leo Septemba 12, 2026, baada ya kufanya ziara ya kukagua hali ya dampo hilo lililopo Pugu, Wilaya ya Ilala, ambapo amesema ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi unaweza kusaidia kukabiliana na changamoto ya mrundikano wa taka katika Jiji la Dar es Salaam.

Amesema wakandarasi wanaohusika na ukusanyaji wa taka mkoani humo wanapaswa kuwa na vifaa na teknolojia zinazokidhi mahitaji ya jiji, ili kuhakikisha taka zinakusanywa na kushughulikiwa kwa ufanisi.
Aidha, Chalamila amewataka wananchi kutekeleza wajibu wao wa kulipa tozo za uondoshaji taka, huku akikemea baadhi ya wazoa taka wanaotupa taka kwenye mito na maeneo yasiyoruhusiwa.

Amesema Septemba 14, atakutana na wadau mbalimbali wa usafi wa mazingira na kutoa maelekezo yatakayolenga kuhakikisha Dar es Salaam inakuwa safi na kudhibiti utupaji taka ovyo.

Katika hatua nyingine, ameiagiza TARURA kuongeza njia za kuingia katika Dampo la Pugu kwa kuboresha na kuchonga barabara, ili kurahisisha magari ya taka kufika katika eneo hilo.
Pia ameshauri vijana wahitimu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kutumika katika utekelezaji wa sheria ndogo za usafi na udhibiti wa utupaji taka hovyo. Aidha, ameelekeza magari ya abiria na maeneo ya wafanyabiashara kuwa na vifaa maalumu vya kutupia taka.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Dampo la Pugu, Richard Kishere, amesema Halmashauri inaendelea na mikakati ya kuboresha miundombinu ya dampo hilo, huku akitaja upungufu wa mitambo kuwa miongoni mwa changamoto zinazokabili eneo hilo.

Ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akiwaapisha Wakuu wa Mikoa wapya, ambapo alisisitiza umuhimu wa kuimarisha usafi katika majiji nchini, ikiwemo Dar es Salaam.